Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WATENDAJI WAKUU OFISI YA RAIS-UTUMISHI WAPIGA KURA, KATIBU MKUU MKOMI ATOA WITO KWA WATUMISHI WA UMMA NA WANANCHI KUJITOKEZA KUTIMIZA HAKI YAO YA KIKATIBA


Watendaji Wakuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora leo tarehe 29.10.2025 wameshiriki zoezi la kupiga kura katika Vituo mbalimbali na kuchagua Viongozi katika ngazi ya Rais, Wabunge na Madiwani.

Akishiriki zoezi hilo katika Kituo cha Kupiga Kura cha Msangalale Mashariki, Kata ya Dodoma Makulu, jijini Dodoma, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ametoa wito kwa Watumishi wa Umma na Wananchi kujitokeza kuchagua viongozi wanaowahitaji kwa maendeleo ya Taifa.

“Namshukuru Mungu nimeshikiri salama zoezi hili muhimu la Kikatiba, nipende kutoa wito kwa Watumishi wa Umma na Wananchi kwa ujumla kushikiriki pia kwani ni haki yao ya msingi.” Bw. Mkomi amesisitiza.

Amesema hali katika Kituo hicho ni ya utulivu na wananchi wamekua wakimiminika kwenda kupiga kura hivyo amewasisitiza kila mwenye haki ya kushiriki zoezi hilo afanye hivyo.

Aidha, Bw. Mkomi amewapongeza Waratibu wa zoezi hilo katika Kituo hicho kwa kuonyesha ushirikiano kwa wananchi wanaoenda kushiriki katika zoezi hilo na kuhakikisha kila mwenye sifa anashiriki kikamilifu.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi hiyo, Bw. Xavier Daudi ameshiriki zoezi hili muhimu katika Kituo cha Mwatano, Kata ya Miyuji, Jijini Dodoma.