Habari
WARATIBU WA JINSIA WATAKIWA KUTOA ELIMU KWA WATUMISHI WA UMMA JUU YA NAMNA YA KUKABILIANA NA VIKWAZO MAHALI PA KAZI

Waratibu wa Jinsia Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma wametakiwa kutoa elimu kwa watumishi wa umma kupitia Wizara zao juu ya namna ya kukabiliana na vikwazo wanavyokutana navyo katika maeneo yao ya kazi ikiwemo uonevu na dhuluma.
Kauli hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Uendelezaji Sera, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cyrus Kapinga alipokuwa akimwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI kufungua kikao kazi kilicholenga kupokea taarifa ya utekelezaji wa mipango kazi ya ujumuishwaji wa jinsia ya Mwaka wa fedha 2024/25 jijini Dodoma.
Bw. Kapinga amesema kuna changamoto ya jinsi ya kutoa taarifa kwani taarifa nyingi hazina maudhui ambayo mtu anaweza kupata picha ya ujumuimuishaji wa masuala ya jinsia katika Utumishi wa Umma.
Aidha, Bw. Kapinga amewataka waratibu hao kutumia kikamilifu muda na nafasi waliyopatiwa na waajiri wao katika kuwasilisha utekelezaji wa mpango kazi kwa weledi na ufasaha pamoja na kupokea maoni na ushauri wa namna bora ya utekelezaji kwa Mwaka wa fedha 2025/26.
Kadhalika, Bw. Kapinga ameishukuru Taasisi ya UONGOZI kwa kuendelea kutoa mafunzo mbalimbali kuhusu programu za Uongozi kwa Wanawake awamu kwa awamu na kuwezesha kufanyika kwa Semina mbalimbali za mwongozo wa ujumuishwaji wa Jinsia katika Utumishi wa Umma kwa Ngazi ya Wizara.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Anuai za Jamii na Mratibu wa VVU, Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Mwanaamani Mtoo amewaasa Waratibu hao kuhakikisha wanatekeleza miongozo mbalimbali inayohusu ujumuishwaji wa jinsia mahali pa kazi kwa ufanisi kama ilivyokusudiwa na Serikali.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI, Kaimu Mkuu wa Idara ya Tafiti na Sera, Bi. Carolina Israel amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI imekuwa ikitoa ushirikiano mkubwa wakati wa mafunzo mbalimbali ya ujumuishwaji wa jinsia mahali pa kazi katika Utumishi wa Umma hivyo, Taasisi ya UONGOZI itaendelea kushirikiana na ofisi hiyo katika kutoa mafunzo hayo kwa ustawi wa maendeleo ya taifa.
Kikao kazi cha Waratibu wa jinsia Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma kinafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 01 hadi 02 Septemba, 2025 katika Ukumbi wa Lounge uliopo katika hoteli ya St. Gaspar jijini Dodoma.