Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAKURUGENZI WA RASILIMALIWATU KUHAKIKI RASIMU YA KANUNI ZA KUDUMU KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, SACP. Ibrahim Mahumi amesema Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma (Standing Order) ni nyenzo muhimu katika Usimamizi wa Utawala na Rasilimaliwatu ndani ya taasisi za Umma.

SACP. Mahumi amesema hayo, wakati akifungua kikao kazi cha wadau kilicholenga kuhakiki Rasimu ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma Toleo la Nne la Mwaka 2025 kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma.

SACP. Mahumi amesema, kupitia Sera ya Menejimenti na Ajira, Sheria ya Utumishi wa Umma Sura 298 na Kanuni zake za 2022 pamoja na miongozo ya Kiutumishi inayotolewa na Serikali ni vitendea kazi muhimuvinavyotumika kusimamia Utumishi wa Umma ili kuwa na ufanisi.

Kupitia kikao kazi hicho SACP. Mahumi amewataka Wakuu wa Idara za Utawala na Utumishi kuona namna ya kutoa maoni na ushauri ili kuboresha zaidi Sera na Kanuni zinazotakiwa kufanyiwa mabadiliko.

Kadhalika, SACP. Mahumi amesema, mabadiliko ya Sera na Kanuni mbalimbali katika Utumishi wa Umma, pia zimeleta mabadiliko katika eneo la Upimaji wa Utendaji kazi ambao awali ulikuwa unajulikana kama (OPRAS) ambayo kwa sasa unajulikama kwa jina la PEPMIS, mabadiliko ya Sheria ya Utumishi wa Umma pamoja na Nyaraka mbalimbali ambazo zinatoa maelekezo tofauti na ya awali ambayo yalikuwa yakifanyiwa kazi.

Akihitimisha hotuba yake, SACP. Mahumi amesema, matokeo ya kikao kazi hicho yalenge katika kutoa mwelekeo chanya wa nyaraka sahihi kupitia Sera na Kanuni zitakazoboreshwa.