Habari
WADAU WASISITIZWA KUIBUA VIGEZO VITAKAVYOKUBALIKA KUFANYA TATHMINI YA MAHITAJI YA RASILIMALIWATU KATIKA ZOEZI LA KUSAFISHA TAARIFA KWENYE MFUMO WA e-MSAWAZO

Ili kuhakikisha takwimu za mahitaji ya watumishi katika taasisi za umma zina uhalisia utakaowezesha maamuzi mbalimbali kuhusiana na rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeandaa mikakati itakayoboresha utekelezaji wa Mfumo wa e-Msawazo ikiwemo kujadili na kukubaliana na wadau wa Mfumo kuhusu vigezo vitakavyotumika katika kutathmini mahitaji ya watumishi zikiwemo Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Hayo yamesemwa leo tarehe 22.09.2025 jijini Dodoma na Mkurugenzi wa Mipango, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Cosmas Ngangaji wakati akimwakilisha Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI kufungua kikao kazi cha siku mbili cha wadau kujadili vigezo vitakavyotumika katika kusafisha takwimu za mahitaji ya Watumishi wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Bw. Ngangaji amesema, Ofisi ya Rais-UTUMISHI inaendelea kuchukua hatua na kuhakikisha Mfumo wa e-Msawazo unaendelea kuwa nyenzo itakayowezesha Serikali kuwa na takwimu sahihi za Watumishi waliopo na wanaohitajika kwa masilahi ya taifa.
“Mfumo wa e-Msawazo unaendelea kuboreshwa ili taarifa zinazopatikana kupitia Mfumo zinaendelea kuwa sahihi zaidi kuwezesha maamuzi mbalimbali ya usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma.” Amesisitiza Bw. Ngangaji.
Bw. Ngangaji amewaelekeza washiriki wa kikao kazi hicho, kutumia vizuri fursa hiyo ili kupata vigezo vitakavyokubalika kufanya tathmini ya mahitaji vitakavyotumika katika zoezi la kusafisha taarifa kwenye Mfumo wa e-Msawazo katika Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kufanya e-Msawazo inakuwa na tija.
Akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Uendelezaji Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda amesema kikao kazi hicho ni mahususi kwa ajili ya wadau ili waweze kujadili tathmini ya mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma kwa lengo la kupata maoni toka kwa wadau hao na kuboresha mfumo huo katika Utumishi wa Umma kwa masilahi mapana ya taifa.
“Tumepata matokeo ya tathmini, sasa kabla ya kuendelea na mchakato mwingine, tumeona ni vema tukakutana na wadau hawa, tumeanza na wadau wa OR -TAMISEMI kutokana na uwingi wa uwakilishi wao katika Utumishi wa Umma.” Ameongeza Bw. Kipanda
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya washiriki, Mwenyekiti wa kikao kazi hicho ambaye ni Afisa Rasilimaliwatu, Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro Bw. Shaban Duru ameahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote yaliyotolewa ili kupata matokeo tarajiwa kama ilivyokusudiwa.