Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

WAAJIRI SERIKALINI WATAKIWA KUZINGATIA WARAKA WA UTUMISHI WA UMMA NA. 5 WA MWAKA 2011 UNAOELEKEZA KUWAPATIA MAFUNZO YA AWALI WATUMISHI WA AJIRA MPYA


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango amewataka waajiri wote katika taasisi za umma kuzingatia Waraka wa Utumishi wa Umma Na. 5 wa mwaka 2011 unaoelekeza waajiri kuwapatia Mafunzo Elekezi ya Awali watumishi wote wa ajira mpya katika utumishi wa umma ndani ya miezi mitatu baada ya kuripoti kazini.

Makamu wa Rais ametoa maelekezo hayo leo kabla ya kuwatunuku wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 39 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.

Amesema Kukosekana kwa mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya kumefanya baadhi ya watumishi kutozingatia miiko ya utumishi wa umma katika utekelezaji wa majukumu yao na ndio sababu kumekuwa na changamoto nyingi za utovu wa nidhamu ikiwemo watumishi hao kujiingiza katika masuala ya rushwa, uvujishaji wa siri za serikali na tabia nyingine zisizofaa.

 

Amesema ni wakati sasa wa waajiri hao kutenga bajeti kwa ajili ya mafunzo ya awali kwa waajiriwa wapya ili waweze kujifunza taratibu za utumishi wa umma na kuepuka changamoto mbalimbali zinazoharibu utumishi wa umma.

Ameutaka uongozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kujipanga kikamilifu kutoa mafunzo hayo ya awali kwa waajiriwa hao wapya pindi watakapojiunga.

Akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Makamu wa Rais kuzungumza na wahitimu hao, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesema Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania ndicho chuo pekee kinachopika watumishi wa umma nchini.

“Mhe. Makamu wa Rais, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, inatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na Chuo hiki cha Utumishi wa Umma maana ndio kitovu cha maarifa na uadilifu katika kuwahdumia wananchi kwa kutumia ujuzi unaotolewa hapa,” Mhe. Simbachawene ameongeza.

Amesema kutokana na umuhimu wa Chuo hicho, watumishi wa umma wote wanapaswa kupitia hapo na kupata mafunzo ya msingi kabla ya kuingia kwenye utumishi wa umma ili wafanye kazi zao kwa uadilifu na kufikia lengo la serikali la kuwa na utumishi wa umma uliotukuka.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Frolens Turuka akizungumza kwa niaba ya Bodi hiyo na Menejimenti ya TPSC, amesema chuo hicho kimejipanga vizuri ili kuendana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia yaliyopo sasa katika dunia.

“Utumishi wa Umma wa sasa umebadilika kulingana na mabadiliko ya teknolojia, hivyo ni jukumu letu kujipanga kikamilifu ili kuendana na mabadiliko hayo ili twende sambamba.” Dkt. Turuka amesisitiza

Akiwasilisha taarifa kuhusu mahafali ya 39 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Kaimu Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Dkt. Ernest Mabonesho amesema jumla ya wahitimu 1,745 kutoka katika kampasi zote sita za TPSC ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Tabora, Singida na Mbeya wametunukiwa vyeti katika ngazi ya shahada, stashahada na astashahada katika kozi mbalimbali.