Habari
“TUWAELEZE WANANCHI MAFANIKIO YALIYOPATIKANA, YALIYOFANYWA NA SERIKALI NI MENGI SANA”-Mhe. Kikwete
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameitaka Menejimenti ya Watumishi Housing Investments (WHI) kuwaeleza wananchi mafanikio yaliyopatikana kwani Serikali imekuwa ikifanya mambo mengi na makubwa lakini wananchi hawajui.
“Mnafanya kazi nzuri sana ya ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma na Wananchi na uwekezaji kupitia Faida Fund, lakini wananchi hawajui, wa kuwaambia wananchi ni sisi, tuwaambie, tuangalie namna ya kutangaza ili wajue” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete ametoa maelekezo hayo leo tarehe 27.11. 2025 akiwa kwenye mwendelezo wa ziara ya kikazi katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo leo ametembelea Watumishi Housing Investments (WHI) jijini Dar es Salaam.
Amesema suala la ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma ni muhimu ili waweze kutekeleza majukumu yao ya kuwahudumia wananchi kwa utulivu na kuweza kuwabakisha watumishi hao katika maeneo yao ya kazi kwani kila mtu anatamani kuishi kwenye mazingira rafiki.
Amesema pamoja na ujenzi wa makazi ya Watumishi, WHI inapaswa kutumia teknolojia ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu na zenye ubora ili Watumishi waweze kununua na kuongeza kuwa kipaumbele kiwe kwenye mikoa ya pembezoni.
“Simamieni msingi ya uanzishwaji wa Taasisi hii wa kujenga nyumba za watumishi kwa gharama nafuu, tufikirie nje ya boksi ili kupata fedha za kujenga nyumba za kutosha na kufikia malengo ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa wananchi badala ya kutegemea zaidi Serikali, bajeti ya
Serikali iwe kichocheo tu,” Mhe. Kikwete amesisitiza. “Mmeyafanya mengi yenye ubunifu, tunaona, mnastahili pongezi kwa mliyoyafanya, kwa mfano kuanzisha Mfuko wa Uwekezaji (Faida Fund) ni ubunifu mzuri, tuendelee kusimamia msingi wa uanzishwaji wa mfuko huu, tujitahidi kutoa elimu ili Watumishi wa Umma wengi zaidi na wananchi wawekeze katika Mfuko huu kwa maisha yao ya sasa na ya baadae pindi wanapohitimisha utumishi wao,” ameongeza.
Amesema ni matamanio ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuona Watumishi wa Umma wanaishi kwenye mazingira mazuri kama ambavyo amekuwa akisisitiza anataka watumishi waishi vizuri ili kuweza kuwahudumia wananchi kwa ubora, “tutafsiri maono yake kwa kuyafanyia kazi,” ameongeza.
Ametoa mfano kuwa WHI inaweza kuingia mkataba wa ujenzi kwa kutumia Halmashauri zenye makusanyo makubwa ya mapato na kujenga nyumba za watumishi, “angalieni Halmashauri inaweza kuchangia kiasi gani na ninyi kiasi gani maana Halmashauri hawawezi kujenga nyumba, muingie katika makubaliano kuona namna gani mnaweza kutekeleza mpango wenu.” Amesisitiza.
Mhe. Kikwete amesema ni wakati sasa wa kuambiana ukweli na sio kuoneeana aibu, “nimeletwa kuja kusaidiana nanyi ili pale mnapokwama tusonge mbele, ndio jukumu lililonileta hapa, tunatamani kuona mabadiliko yanaonekana, tuongeze kasi ya wawekezaji katika Mfuko huu wa Faida Fund kwa kujitangaza zaidi,” amesisitiza.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda, akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Waziri kuzungumza na Menejimenti ya WHI amesema kitendo cha Waziri kufanya ziara katika taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ni fursa kubwa kwa Watendaji wa taasisi hizo kuboresha utendaji.
“Mhe. Waziri amerudi kwa kofia nyingine ya juu zaidi hivyo, kutembelea taasisi zilizo chini ya Ofisi yake ni fundisho kwa Viongozi wa Taasisi na hata kwetu sote kwani tunapata fursa ya kusikiliza matamanio yake ili kuona namna bora ya kufanya vizuri zaidi katika utekelezaji wa majukumu yetu kwa ustawi wa taifa.” Bw. Kipanda ameongeza.
Amesema kila anachozungumza Mhe. Waziri kinagusa Watumishi wa Umma na wananchi akitolea mfano wa ujenzi wa makazi ya watumishi na uwekezaji kupitia Mfuko wa Faida Fund kuwa ni kazi yake ya kisera.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji, Kaimu Mkurugenzi wa Watumishi Housing Investments (WHI) Bw. Sephania Solomon amemshukuru Mhe. Kikwete kwa ushauri na maelekezo aliyoyatoa ambapo ameahidi kuyafanyia kazi.
