Habari
TUMIENI KWA UFASAHA VITENDEA KAZI VILIVYOTOLEWA NA SERIKALI KUTEKELEZA JUKUMU LA KUPAMBANA NA RUSHWA-Mhe. Simbachawene

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene amesisitiza watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa Tanzania (TAKUKURU) kutumia kikamilifu vitendea kazi ambavyo serikali imekuwa ikiwapatia ili kuhakikisha kazi ya kupambana na rushwa inatekelezwa kwa ufasaha.
Mhe. Simbachawene ametoa kauli hiyo leo tarehe 26 Oktoba, 2024 katika Shule ya Polisi-Moshi alipokuwa akitoa maelezo ya awali kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa kufunga mafunzo ya awali kwa watumishi wapya 436 wa TAKUKURU.
Mhe. Simbachawene amesema katika kuhakikisha rushwa inatokomezwa nchini, Serikali imekuwa ikifanya jitihada mbalimbali ikiwemo kujenga Ofisi za TAKUKURU mikoani na wilayani, kuajiri watumishi na kutoa vitendea kazi, hivyo hakuna kisingizio tena kwa watumishi hao kutofanya kazi kwa ufasaha.
“Hakuna kisingizio tena, ninyi leo mmekuwa mashahidi na kuona Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa alivyokuwa akikabidhi magari kwa ajili ya utekelezaji wa majukumu yenu ya kupambana na rushwa, hivyo mkavitendee haki vitendea kazi hivyo kwa kufanya kazi kwa bidii na uadilifu” Mhe. Simbachawene.
Waziri Simbachawene amemuahidi Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa kuwa yeye pamoja na watendaji wa Ofisi yake wataendelea kuisimamia kikamilifu taasisi hiyo na kuvitumia vizuri vitendea kazi wanavyopatiwa katika jukumu la kuzuia na kupambana na rushwa.
Waziri Simbachawene amemshukuru Waziri Mkuu kwa kufunga mafunzo hayo na kuwapongeza wahitimu pamoja na wote walioshiriki katika kufanikisha mafunzo hayo ya Maafisa Uchunguzi na Wachunguzi Wasaidizi.
Mafunzo hayo yaliyolenga kuwaandaa watumishi wa TAKUKURU kutekeleza majukumu yao kwa uzalendo, uadilifu, weledi, uwajibikaji na ushirikiano yamefanyika kwa muda wa miezi mitano (5) na yamefungwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.