Habari
TUJIKITE KUFUNDISHA KOZI ZITAKAZOENDA KUTATUA CHANGAMOTO ZA WAHITIMU NA WANANCHI-Mhe. Kikwete
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameielekeza Bodi ya Ushauri na Menejimenti ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kujikita zaidi katika kufundisha kozi zitakazoenda kutatua changamoto za wahitimu na wananchi kwa ujumla.
Waziri Kikwete ametoa maelekezo hayo leo tarehe 28 Novemba, 2025 kabla ya kuwatunuku wahitimu wa kozi mbalimbali katika mahafali ya 42 ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Mhe. Kikwete amesema, Watanzania wanahitaji kupata elimu ya kuwasaidia katika maisha yao na sio ya kukaa na vyeti ndani. “Naielekeza Bodi na Menejimenti kuhakikisha Kozi tunazoanzisha zinaleta majawabu ya changamoto za Watanzania,” Mhe. Kikwete amesisitiza.
Mhe. Kikwete amesema anayo maswali ya msingi ya kujiuliza, akitolea mfano wa Kozi ya Makatibu Mahususi, je Kozi zilizotolewa kwa watumishi hawa zamani zinafanana na zinazotolewa sasa? Tumeshuhudia uvunjifu wa maadili kwa watumishi. Ni wajibu wetu kuhakikisha watumishi wanakuwa na uadilifu, tutengeneze Utumishi wa Umma wenye weledi. Je watumishi wa umma bado ni wazalendo? Ni majibu yanayopatikana kwa Menejimenti na Bodi ya Chuo hiki. Tuangalie Mitaala ili ijibu maswali yangu,” amesisitiza.
Aidha, ametoa wito kwa Wahitimu kuendelea kujifunza hata baada ya kuhitimu, kwani dunia ya leo inahitaji kujifunza maisha yote ili kuendelea kuwa na uwezo wa kukidhi mahitaji yanayobadilika kila uchwao.
“Nawasihi mjiepushe na vitendo vyovyote vinavyoweza kuharibu taswira yenu na ya Utumishi wa Umma, kama vile rushwa, uzembe, ubaguzi, matumizi mabaya ya madaraka na kutowajibika. Badala yake, muwe mfano wa kuigwa katika weledi, uwajibikaji, uadilifu na kujituma kazini,” ameongeza
“Leo mmehitimu, na baadhi yenu kesho mnatarajiwa kuwa viongozi na watendaji katika sekta mbalimbali. Taifa linawategemea hivyo mtakapopata fursa ya kuajiriwa mkawe mabalozi wa Chuo cha Utumishi wa Umma kwa kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Maadili ya Utumishi wa Umma” amesema.
Mhe. Kikwete amesema ni matarajio ya Serikali kwamba Chuo hiki kitaendelea kuwa chachu ya mabadiliko katika utumishi wa umma kupitia mafunzo ya muda mfupi, tafiti zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali katika utumishi wa umma pamoja na ushauri wa kitaalamu zinazotolewa kwa taasisi za umma na sekta binafsi. Serikali itaendelea kushirikiana na uongozi wa chuo kuhakikisha kuwa bajeti ya maendeleo inaendelea kutengwa mwaka hadi mwaka.
Akiwasilisha hotuba ya Katibu Mkuu-UTUMISHI kabla ya kumkaribisha Waziri Kikwete kuzungumza na wahitimu hao, Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Nolasco Kipanda amewapongeza wadau wote waliofanikisha Chuo hiki kuendelea na kuwapongeza pia wahitimu kwa kutunukiwa vyeti na kuwasisitiza kuitumia vyema elimu waliyoipata.
Amesema Serikali imeendelea kukijengea uwezo Chuo cha Utumishi wa Umma kupitia miradi ya kimkakati yenye tija.
Kufuatia hotuba hiyo ya Katibu Mkuu, Dkt. Turuka, amepongezwa kwa kuteuliwa kwa mara nyingine kuwa Mwenyekiti wa Bodi hiyo kwani inaonyesha uongozi wake mahiri, uadilifu na usimamizi madhubuti aliouonyesha.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania, Dkt. Frolens Turuka akizungumza kwa niaba ya Bodi hiyo na Menejimenti ya TPSC, amewapongeza wahitimu wote waliomaliza salama na kutunukiwa vyeti na kutoa wito wa kutumia vema maarifa waliyoyapata wakati wote wa masomo yao kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla.
Amesema wao kama Bodi ya Ushauri ya Chuo hicho wataendelea kushauri ipasavyo ili kujenga uwezo wa Sekta ya Umma kulingana na mabadiliko ya teknolojia na kutekeleza yale yanayopaswa kufanywa katika Utumishi wa Umma.
Akiwasilisha taarifa ya utendaji wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) Mtendaji Mkuu na Mkuu wa TPSC, Dkt. Ernest Mabonesho amesema jumla ya wahitimu 6956 kutoka katika kampasi zote sita za TPSC ambazo ni Dar es Salaam, Tanga, Mtwara, Tabora, Singida na Mbeya wametunukiwa vyeti katika ngazi ya shahada, stashahada na astashahada katika kozi mbalimbali.
Dkt. Mabonesho amesema Mahafali hayo ni miongoni mwa matukio muhimu yanayoashiria maendeleo ya chuo hicho ambacho tangu kilipoanza mpaka leo kinatimiza miaka 25. “Mhe. Mgeni Rasmi, kufanyika kwa mahafali ya leo sio tukio la kawaida tu bali ni maendeleo na uvumilivu tangu kuanzishwa kwake kama Wakala ya Serikali. Tulianza na Kampasi mbili lakini sasa ziko sita, jambo lililoongeza fursa za mafunzo kwa wahitaji kwani kozi pia zimeongezeka katika taaluma mbalimbali ikiwemo mafunzo kwa njia ya mtandao,” Dkt. Mabonesho ameongeza.
