Habari
TIMU YA MPIRA WA PETE OFISI YA RAIS - UTUMISHI YAFUZU KUINGIA ROBO FAINALI

Timu ya mpira wa pete ya Ofisi ya Rais - UTUMISHI na Utawala Bora imefanikiwa kufuzu kuingia hatua ya robo fainali katika mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) yanayoendelea jijini Mwanza.
Utumishi imejihakikishia nafasi hiyo baada ya kuibuka na ushindi wa magoli 61 dhidi ya timu ya Mashtaka ambao walipata goli 4 katika mchezo huo wa hatua za Kumi na Sita Bora (Mtoano), jambo lililodhihirisha nidhamu, umoja na maandalizi madhubuti ya kikosi hicho.
Kocha wa timu hiyo, Esther Halla, amepongeza timu yake na akibainisha kuwa matokeo hayo ni ishara ya kujituma na kujiamini kwa timu nzima. Aidha, amewataka wachezaji kuongeza bidii zaidi ili kuhakikisha wanavuka hatua ya robo fainali na kufikia fainali ya mashindano hayo.
Mashindano ya SHIMIWI 2025 yameendelea kuvutia hisia na msisimko mkubwa kutoka kwa mashabiki na watumishi, yakilenga kuimarisha mshikamano, kujenga afya na kuendeleza mshindano ya michezo miongoni mwa Wizara na Taasisi za Serikali.