Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TASAF YAPONGEZWA KWA UJENZI WA STENDI YA KISASA SONGEA


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya Wajumbe wa kamati hiyo amefurahishwa na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi kwa fedha kidogo.

Mhe. Dkt. Mhagama ameyasema hayo tarehe 14 Machi, 2024 katika Kijiji cha Lundusi kata ya Peramiho katika halmashauri ya Wilaya ya Songea wakati wa ziara ya kamati hiyo ya kukagua utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali.

“Nikiangalia nyuso za wanakamati zinanipa ishara ya kuwa wameridhika na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa stendi ya kisasa ya mabasi kwa kuwa unapofika katika eneo la mradi huu unaanza kuona moja kwa moja thamani ya fedha ya umma” amesema Mhe. Dkt. Mhagama.

Aidha, Mhe. Dkt. Mhagama amewapongeza viongozi na watendaji wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa kuisimamia vizuri TASAF na kuhakikisha jitihada kubwa zinazofanywa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kutafuta fedha na kuhudumia wananchi wake zinafanyika kwa ufanisi.

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete ameieleza na kuihakikishia Kamati hiyo kuwa hakuna kitu kitakachopungua katika mradi na atahakikisha TASAF inasimamiwa ipasavyo hadi kukamilika kwa mradi huo.


Mhe. Kikwete afafanua kuwa mradi huo wa  kisasa wa stendi ya mabasi uliibuliwa na wananchi wenyewe wa Kijiji cha Lundusi mwaka 2022 kupitia mkutano wao halali wa jamii ambapo walimuomba fedha Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia TASAF waweze kujengewa stendi hiyo.

“Mheshimiwa Mwenyekiti kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene  tunashukuru Kamati yako kwa kupitisha maombi ya bajeti ya ujenzi wa stendi hiyo na huu ndio utekelezaji wa bajeti hiyo. Mradi huu utaongeza uchumi na kipato kwa Wanaperamiho na Songea kwa jumla” aliongeza Mhe. Kikwete.

Hadi kukamilika kwa mradi huu, kituo cha mabasi kitakuwa na maduka 36, vibanda vya walizi, kituo cha polisi, matundu 8 ya vyoo na uzio.