Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TASAF KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO MKOANI NJOMBE


Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama kwa niaba ya Wajumbe wa kamati hiyo amefurahishwa na namna TASAF ilivyojenga jengo la kuhudumia mama na mtoto kutokana na fedha ambazo zinatolewa na Serikali ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mhe. Dkt. Mhagama amesema kuwa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni Mama na anajali afya ya mama na mtoto mathalani ameleta fedha nyingi na kujenga jengo ambalo ni muhimu sana kwa ustawi wa jamii ya wana Njombe na watanzania wote kwa jumla.

“Mimi pamoja na kamati yangu tumeridhika na ujenzi wa jengo hili la kuhudumia mama na mtoto katika Hospitali ya Halmashauri ya Mji wa Njombe na tunaomba jengo hili litumike kama mfano kwa Halmashauri nyingine hapa nchini” ameongeza Mhe. Mhagama.

Aidha, amefafanua kuwa ujio wao wa kukagua miradi ya maendeleo ni maelekezo ya Kiti cha Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye anakiu ya kujua iwapo fedha zinazoombwa na Wizara na kupitishwa na Bunge kwa lengo la utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini zinafika katika maeneo husika na kutatua changamoto za wananchi.

Vilevile,  Mhe. Mhagama ameipongeza TASAF kwa kuendelea kutekeleza miradi ambayo inaacha alama ya kudumu kwa jamii na taifa kwa jumla. Pia, kwa kufanya kazi kubwa ya kunusuru kaya maskini katika nyanja mbalimbali ikiwa ni pamoja na elimu, miundombinu ya barabara na afya bila ubaguzi wa kiitikadi kwa wananchi.  

Naye, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais Menejimeti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewasihi wana Njombe kutambua kuwa ujauzito ni baraka kutoka kwa Mungu na sio ugonjwa, hivyo watumie fursa ya kukamilika kwa jengo hilo ili kupata huduma ya mama na mtoto ikiwa ni pamoja na Watoto ambao wamezaliwa kabla ya muda (Watoto njiti) na wale wenye uzito mdogo.

Pia, Mhe. Kikwete amempongeza Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu kwa kuleta vifaa tiba katika hospitali hiyo ya Halmashauri ya Mji wa Njombe ili kuendelea kuokoa afya ya mama na mtoto.

Mhe. Kikwete ametoa rai kwa wananchi wote wa Mkoa Njombe kushirikiana katika utunzaji wa jengo na miundombinu yake ili iweze kunufaisha wananchi wote.