Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TANZANIA YANG’ARA TUZO ZA KIMATAIFA ZA UBUNIFU WA MFUMO WA KIDIJITALI WA eMREJESHO


Tanzania imeng'ara katika tuzo za Kimataifa za ubunifu wa mfumo ya kidijitali wa Mrejeshoi (e-Mrejesho) uliosaidia kuleta mageuzi makubwa katika  uboreshaji wa utoaji wa  huduma kwa wananchi.

Tuzo hizo zimetolewa jana nchini Korea Kusini na Shirika la Umoja wa Mataifa (UN) wakati wa Mkutano wa Umoja wa Jukwaa la Umoja wa Mataifa la Tuzo za Utumishi wa Umma (2024 UN Public Service Awards (UNPSF).

Tuzo hiyo iliyopokelewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Bw.  Xavier Daudi ambapo nchi 15 kati ya 72 zimetunukiwa tuzo hizo huku kwa upande wa Afrika, Tanzania na Afrika ya Kusini ndizo zilizotambuliwa katika tuzo hizo.

Akizungumza mara baada ya kupokea tuzo hiyo, Naibu Katibu Mkuu, Bw. Daudi amesema Tanzania imepokea tuzo kwenye kipengele cha ubunifu kwenye Taasisi za Umma (Honorable Mention Innovation in Public Institution).

‘‘Tuzo tuliyoipokea ni heshima kubwa na pia ni fahari kwa vijana wetu wazawa waliobuni mfumo huo ambao wananchi wana uwezo wa kuiambia Serikali yao kwamba utumishi wa umma una uimara na ulegevu katika utoaji huduma’’ amesema

Katika mkutano huo ujumbe wa Tanzania umeongozwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi pamoja na Wakurugenzi kutoka Ofisi hiyo akiwemo Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Maadili Bi. Leila Mavika, Mkurugenzi wa Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Serikalini, Bw. Priscus Kiwango pamoja na Mkurugenzi, Mhandisi Rico Bomani na Meneja wa Mafunzo na Ubunifu, Mhandisi Jaha Mvula kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA).

Aidha Mhe. Balozi Togolani Edris Mavura, Balozi wa Tanzania nchini Korea ya Kusini aliambatana na ujumbe huo katika kupokea tuzo.