Habari
TAASISI ZAPONGEZWA KUSIMAMIA MIENENDO YA KIMAADILI KATIKA UTUMISHI WA UMMA

Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI ambaye ni Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa ofisi hiyo, Bibi Hilda Kabissa amepongeza Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma kwa kuendelea kusimamia tabia na mienendo ya kimaadili ya watumishi wanaowasimamia.
“Ninawapa pongezi kwa kuwa mmetoa mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi wenu mahala pa kazi ili waweze kuzingatia maadili katika utoaji wa huduma kwa umma” alisema Bibi Hilda.
Bibi. Kabissa ametoa pongezi hizo wakati akifungua kikao kazi cha sita (6) cha kubadilishana uzoefu na taarifa baina ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma kilichofanyika katika Ukumbi wa Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira jijini Dodoma.
Bibi. Kabisa aliongeza kuwa pongezi hizo anazowapa viongozi wa taasisi hizo ziwe chachu ya kuongeza ubunifu zaidi na kuweka mikakati endelevu ya kuboresha misingi ya maadili ya utendaji na maadili ya kitaaluma, ili kuimarisha utendaji kazi Serikalini”.
Vilevile, alibainisha kuwa kazi ya kusimamia maadili ya watumishi wa umma si rahisi lakini kwa kuwa taasisi hizo ziliwajengea uwezo watumishi wao, imekuwa kazi rahisi kwao kusimamia maadili kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo hivyo kupunguza vitendo vya rushwa kwa watumishi wa umma katika utoaji wa huduma.
Kadhalika, Bibi. Kabissa amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kuboresha mbinu mbalimbali za usimamizi na utatuzi wa changamoto wanazokutana nazo katika usimamizi wa maadili kwa watumishi wa umma ili kuleta ustawi wa wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bi. Felister Shuli akitoa maelezo ya awali amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ina jukumu la kusimamia maadili ya utendaji katika Utumishi wa Umma, ambapo njia mojawapo ya utekelezaji wa jukumu hilo ni kushirikiana na wadau mbalimbali wanaohusika na usimamizi wa maadili zikiwemo Taasisi Simamizi za Maadili ya Utendaji pamoja na Mamlaka Simamizi za Maadili ya Kitaaluma.
Mkurugenzi Shuli amesema, katika kikao kazi hicho wanatarajia kufundishwa mada tano (5) zitakazoakisi Usimamizi wa Maadili ya Utendaji, na Maadili ya Kitaaluma katika Utumishi wa Umma.