Habari
TAASISI ZA UMMA KUFANYA UHAKIKI WA TAKWIMU ZA WATUMISHI WA UMMA WENYE VVU, UKIMWI NA MAGONJWA SUGU YASIYOAMBUKIZA
Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI Bw. Cyprus Kapinga amezitaka Wizara na Taasisi za Umma kufanya uhakiki wa takwimu za watumishi wa umma wenye VVU, Ukimwi na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) ili kulinda afya za watumishi hao.
Bw. Kapinga ametoa wito huo leo wakati akifungua kikao kazi cha Robo ya Nne ya Mwaka 2023/2024 kilichoshirikisha Kamati ya Kifaifa, Waratibu wa Wizara wa Kudhibiti VVU, Ukimwi na Magonjwa Yasiyoambukiza (MSY) pamoja na Wajumbe, Wenyeviti, Makatibu wa Mkoa wa Manyara wanaosimamia magonjwa hayo.
“Tunatakiwa kuwa na takwimu sahihi ya watumishi hao ili kurahisisha zoezi la kupanga bajeti ya kuwahudumia na kuimarisha afya ya akili na kudhibiti msongo wa mawazo. Watumishi hao ni sehemu ya nguvu kazi ya Taifa inayohudumia wananchi” alisisitiza Bw. Kapinga.
Aidha, Bw. Kapinga ametoa rai kwa Maafisa Masuuli wote katika taasisi za umma kuunda na kuimarisha Kamati za VVU, Ukimwi na Magonjwa Sugu Yasiyoambukiza (MSY) zilizopo kwa kutoa nafasi kwa wanakamati hao kupata mafunzo na elimu itakayowafanya wawe na uwezo wa kushawishi watumishi kupima afya na hivyo kuwa na takwimu sahihi kwa mipango bora na endelevu.
Awali akitoa neno la utangulizi, Katibu Tawala Mkoa wa Manyara, Bi. Maryam Muhaji aliwataka washiriki wa kikao kazi hicho kusikiliza na kufuatilila kwa makini mada zote zitakazowasilishwa ili wapate uwezo na ujuzi Madhubuti wa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kupitia Idara ya Uendelezaji Sera ipo mkoani Manyara kwa lengo la kujadili utekelezaji wa mapambano dhidi ya VVU, Ukimwi na Magonjwa yasiyoambukiza (MSY) ili kuwalinda watumishi wa umma na kuhakikisha taifa linaondokana na vifo vitokanavyo na magonjwa hayo ifikapo mwaka 2030.