Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

TAASISI ZA SERIKALI ZAELEKEZWA KUANZISHA QR CODE ILI KUTOA MREJESHO WA HUDUMA WANAZOZITOA KWA WANANCHI


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amezielekeza Taasisi za Serikali kuanzisha Msimbo Mraba (QR CODE) utakaowezesha kutoa mrejesho wa huduma zinazotolewa na Taasisi hizo kwa wananchi.

Bw. Mkomi ametoa maelekezo hayo leo alipokuwa akifungua kikao kazi cha wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kuhusu matumizi na usimamizi wa Mfumo wa Kielekroni (e-Mrejesho) Toleo la Pili kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.

Bw. Mkomi amesema ushughulikiaji wa huduma za mrejesho zinazotolewa na Serikali ni utaratibu uliowekwa mahususi kwa lengo la kuimarisha uwajibikaji na usikivu ndani ya Taasisi za Umma pamoja na kukuza misingi ya Utawala Bora.

Katibu Mkuu Mkomi amewataka wasimamizi wa Rasilimaliwatu katika Taasisi hizo kuwa na uelewa wa pamoja katika kutoa huduma na kuona namna ya kupata mrejesho kwa jinsi inavyowaridhisha wahusika katika Utumishi wa Umma.

Vilevile, Bw. Mkomi amewataka washiriki wa kikao kazi hicho kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mfumo wa e-Mrejesho katika taasisi zao ili waweze kutoa elimu hiyo kwa watumishi wengine waliopo katika taasisi zao kwa lengo la kuimarisha utendaji kazi.

Kadhalika, Bw. Mkomi ameongeza kuwa ili kuboresha utekelezaji huo wa Mfumo wa e-Mrejesho amewataka Maafisa Tehama kutengeneza QR CODE kwenye taasisi zote ili kuwezesha wananchi kuutumia na kupeleka malalamiko yao au mrejesho kwenye taasisi husika  

“Katika wananchi 100 hautakosa wananchi 60 wenye simu za kupangusa hivyo, huduma hiyo ya       QR CODE kwa asilimia 60 itaenda mbali zaidi kwa muda mfupi,’’ amesema Bw. Mkomi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Usimamizi wa Maadili, Bi. Felista Shuli amesema lengo la kikao kazi hicho ni washiriki kuwezeshwa, kupitishwa na kujadili kwa pamoja kuhusu usimamizi na utekelezaji wa mfumo wa mrejesho ambao ni mojawapo ya mifumo iliyowekwa na Serikali kwa lengo la kusimamia uwajibikaji katika Utumishi wa Umma.

Akitoa neno la shukrani kwa mgeni rasmi ambaye ni Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bw. Michael John amemuahidi Katibu Mkuu Mkomi kuwa watazingatia maelekezo yote ambayo ameyatoa ili waweze kuboresha utendaji kazi kwa ustawi wa Taifa.