Habari
SIMBACHAWENE AWAASA WAHITIMU TPSC KUSIMAMIA NA KUTUNZA MAADILI YA TAALUMA WALIZOSOMEA KWA USTAWI WA TAIFA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewaasa wahitimu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania (TPSC) kusimamia na kutunza maadili ya taaluma walizosomea kwa ustawi wa taifa.
Mhe. Simbachawene amesema hayo leo tarehe 30 Mei, 2025 kwenye Mahafali ya 41 ya kuwatunuku wahitimu wa ngazi mbalimbali wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa Social Rwoma RC Mission mkoani Singida.
“Kuhitimu ngazi za Shahada, Stashahada na Astashahada katika fani mbalimbali sio jambo dogo, elimu mliyoipata ni kubwa, hakikisheni mnasimamia na kutunza maadili ya elimu hiyo kwa manufaa yenu na ustawi wa taifa” amesisitiza Mhe. Simbachawene.
Mhe. Simbachawene amewataka wahitimu walioajiriwa katika Utumishi wa Umma na watakaoajiriwa kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo ya Utumishi wa Umma ikiwa ni pamoja na kutunza siri za Serikali na kuepuka rushwa katika utekelezaji wa majukumu yao na wahitimu ambao hawana ajira kutumia ujuzi walioupata kujiajiri kwa maendeleo ya taifa.
Aidha, ametoa rai kwa wahitimu hao kutunza afya zao pamoja na kuepuka Magonjwa Yasiyoambuza kwa kuwa taifa linawahitaji katika kukuza uchumi wa nchi.
Vilevile, Mhe. Simbachawene ameueleza uongozi wa chuo hicho kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ina matarajio makubwa na Chuo hicho kwa kuwa kimeimarika sana hasa katika kuwajengea uwezo watumishi wa Umma na kutoa wahitimu mahiri na wenye uzalendo wanaoleta chachu ya maendeleo nchini.
Kadhalika, Mhe. Simbachawene amewapongeza Walimu, Wazazi na Walezi wa wahitimu hao kwa jitihada kubwa ambazo kila mmoja kwa nafasi yake amezifanya ili kufanikisha kupata wahitimu hao wa ngazi za Shahada, Stashahada na Astashahada katika fani mbalimbali.
Awali, Mkuu wa Chuo na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania Dkt. Ernest Mabonesho amemshukuru Waziri Simbachawene kwa kukubali mwaliko wa kuwa mgeni rasmi katika mahafali hayo na kumtaarifu kuwa jumla ya wanafunzi 1330 wamehitimu kozi mbalimbali katika chuo hicho wakiwemo wanawake 906 na wanaume 224.
Dkt. Mabonesho ameongeza kuwa pamoja na jitihada nyingine zinazofanywa na chuo hicho, wameendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali za ndani ikiwemo Chuo cha Hombolo na vyuo vingine mbalimbali pamoja na vya nje ya nchi kwa lengo la kuboresha ujuzi na kubadilishana uzoefu katika utendajikazi.
“Mhe. Mgeni rasmi tumefanya jitihada mbalimbali ili kuboresha mafunzo yetu kwa kushirikiana na vyuo vingine vya ndani na nje ya nchi hasa vinavyohusika na masuala ya Utumishi wa Umma ikiwemo chuo cha Hombolo pamoja na vyuo vingine ili kuweza kupata fursa ya kujifunza na kuboresha utendajikazi” alisema Dkt. Mabonesho.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, SACP. Ibrahim Mahumi amesema taifa limepata wahitimu ambao ni nguvukazi nyingine watakaosaidia utendajikazi katika Utumishi wa Umma na taifa kwa ujumla.
Aidha, SACP. Mahumi amemshukuru na kumpongeza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene kwa kusimamia miongozo mbalimbali pamoja na taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo ambayo imekisaidia Chuo cha Utumishi wa Umma Tanzania kuhitimisha wanafunzi wanaoweza kutekeleza majukumu mbalimbali pasipokuwa na changamoto zozote.