Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

SERIKALI YAWEKA MKAZO UJUMUISHWAJI WA HAKI ZA KIJINSIA KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili, ametoa wito kwa Taasisi za Umma kuhakikisha masuala ya kijinsia yanajumuishwa katika utekelezaji wa majukumu yao ili kujenga utumishi wa umma unaozingatia usawa, haki na fursa kwa wanawake na wanaume.

Bi. Lwangili ameyasema hayo Septemba 15, 2026 jijini Dodoma wakati akifungua Kikao Kazi cha siku mbili cha Waratibu wa Jinsia Mahali pa Kazi katika Utumishi wa Umma, kinacholenga kujadili na kuimarisha utekelezaji wa masuala ya kijinsia katika maeneo ya kazi.

Amesema Mwongozo wa Ujumuishaji wa Haki za Kijinsia katika Utumishi wa Umma wa mwaka 2023 umeandaliwa kuwa nyenzo muhimu ya kutoa mwelekeo kwa Taasisi za Umma kuhusu namna ya kujumuisha masuala ya kijinsia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.

Ameeleza kuwa utekelezaji wa Mwongozo huo unapaswa kuangaliwa katika muktadha mpana wa kufanikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, ambayo imeweka azma ya kuifanya Tanzania kuwa kinara barani Afrika na miongoni mwa nchi 10 bora duniani katika kupunguza pengo la kijinsia kwa asilimia 85.

Aidha, Bi. Lwangili amesema Ofisi ya Rais – Utumishi imeendelea kuchukua hatua kuhakikisha maeneo ya kazi yanakuwa salama, jumuishi na yenye kutoa fursa sawa kwa wanawake na wanaume kushiriki katika nafasi za uongozi na kufanya maamuzi.

Amesisitiza kuwa ushiriki wa wanawake na wanaume katika uongozi na maamuzi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali, hivyo Waratibu wa Jinsia wanapaswa kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi ili kuhakikisha masuala ya kijinsia yanazingatiwa katika mipango, sera, programu na shughuli za Taasisi za Umma.