Habari
OFISI YA RAIS YAAHIDI KUONGEZA KASI KATIKA UTOAJI WA HUDUMA KWA UMMA

Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu-Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Musa Magufuli amesisitiza kuwa ofisi hiyo itaongeza kasi zaidi ya utoaji wa huduma bora kwa umma.
Msisitizo huo ameutoa leo Oktoba 1,2025 wakati watumishi wa Idara yake walipokuwa na kazi maalumu ya kupokea wateja wa ndani na nje ya ofisi hiyo ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika katika ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.
“Sisi kama Ofisi ya Rais-UTUMISHI tunawajibika kuwa na weledi na kuzingatia uadilifu katika utoaji wa huduma kwa umma wakati wote” alisema Magufuli.
Aidha, Bw. Magufuli aliongeza kuwa ofisi hiyo itaendelea kuimarisha mifumo ya utoaji huduma, ikiwemo matumizi ya mifumo ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.
Maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja hufanyika kila mwaka duniani kote, kwa lengo la kuhimiza taasisi mbalimbali kuongeza ubunifu na ubora katika kuwahudumia wateja wao.