Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

OFISI YA RAIS-UTUMISHI YATEKELEZA AHADI YA RAIS YA KUAJIRI VIJANA NDANI YA SIKU 100


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema Serikali kupitia Ofisi yake imetekeleza ahadi ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuajiri vijana 12,000 ndani ya siku 100 za kwanza za kipindi cha pili cha awamu ya sita.

Waziri Kikwete amesema hayo wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa siku 100 za ahadi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan uliofanyika Januari 30, 2026 katika Ukumbi wa Habari Maelezo jijini Dodoma.

Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliahidi kuajiri vijana 5,000 kwa sekta ya Afya na watumishi 7,000 kwa sekta ya elimu ambao ni Walimu wa Masomo ya Sayansi na Hisabati.

Mhe, Kikwete alisema kuwa hadi tarehe 20 Januari, 2026 watumishi hao wapya wamepatikana na wamepangiwa vituo na barua za ajira zimetumwa moja kwa moja kwenye akaunti za waombaji hao na wamesharipoti katika vituo vyao vya kazi.

“Kwa sasa mambo yote yanakwenda kidijiti ambapo watumishi hao wapya wamepokea barua zao za ajira kwa njia ya simu za mkononi na wameripoti kwenye vituo vyao vya kazi na waliowahi kabla ya kutuma taarifa za mishahara wamepokea mshahara wao wa kwanza mwezi huu wa Januari” Mhe. Kikwete aliongeza.

Aidha Mhe. Kikwete ametoa wito kwa waajiriwa wapya ambao bado hawajaripoti katika vituo walivyopangiwa kufanya hivyo ndani ya siku 14 tangu walipopokea barua ya kazi, kinyume na hapo nafasi zao zitachukuliwa na wasailiwa wengine ambao wapo katika kanzi data.

Mh. Kikwete ametoa wito kwa Vijana wa kitanzania kuwa kwa wale wote wenye sifa wasisite kuomba nafasi za ajira pindi zitakapotangazwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma kwani Serikali bado itaendelea kutangaza nafasi hizo.

Kadhalika Mhe. Kikwete amesema, katika kutekeleza ahadi za siku 100 za Mhe. Rais, Dkt Samia Suluhu Hassan, Ofisi ya Rais, Menejiementi ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imeboresha Mfumo wa kielektroniki wa e-Mrejesho ambapo Wananchi wanaweza kuwasilisha maoni au malalamiko kupitia mfumo huo ili kuimarisha Utawala Bora.

Mhe. Kikwete amehitimisha kwa kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan  kwa kutoa maelekezo ya kuhakikisha vijana wanapata ajira ili kuongeza wigo wa kutoa huduma kwa umma.