Habari
OFISI YA RAIS MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA YASHIRIKI BONANZA LA UZINDUZI MASHINDANO YA SHIMIWI 2025.

Na Eric Amani, Dodoma
Ofisi ya Rais - UTUMISHI imeshiriki Bonanza la Uzinduzi wa Mashindano ya Shirikisho la Michezo la Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) yanayotarajia kuanza Septemba 1 hadi 16, 2025 Jijini Mwanza.
Bonanza hilo limefanyika (Agosti 2, 2025) katika Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na watumishi wa Wizara na Idara za Serikali zinazojitegemea.
Akifungua bonanza hilo Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu, Ndugu Mululi Majula Mahendeka ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Mhe. Balozi Dkt. Moses Kusiluka, amewapongeza viongozi na watumishi wote waliojumuika katika bonanza hilo.
Aidha, amewakumbusha viongozi na watumishi wa serikali wajibu wao wa kutoa huduma bora kwa wananchi huku akisisitiza kuwa wajibu huo utatekelezwa ipasavyo endapo watumishi hao watakuwa na afya njema.
“Ili kutekeleza majukumu yao ya msingi, watumishi wa umma wanahitajika kuwa na afya njema ambayo inajengwa kwa kula milo bora, kufanya uchunguzi wa afya mara kwa mara, kujiepusha na matumizi ya pombe na sigara, msongo wa mawazo pamoja na kujihusisha na mazoezi,” ameeleza Ndugu Mahendeka na kuongeza
“Michezo sio burudani tu bali ni shughuli muhimu yenye mchango mkubwa kiuchumi, kijamii, kiafya na kitaalum. Michezo ni sehemu ya kazi hivyo Wakuu wa Taasisi waone umuhimu wa kutenga bajeti kwa ajili ya michezo na kutoa vibali kwa watumishi kushiriki michezo mbalimbali”.
Pia Ndugu Mahendeka amewakumbusha watumishi wa umma kutoa huduma bora kwa watanzania kwa kuwa ndio msingi muhimu wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi na ili huduma iwe bora jumuishi na endelevu ni vyema kuzingatia upatikanaji wake, ubora uwazi na uwajibikaji, muda na ufanisi.
Amesisitiza kuwa, huduma zitolewe kwa wakati bila usumbufu au ucheleweshaji, heshima kwa wateja ushirikishwaji kwa wananchi bila kusahau teknolojia na ubunifu na kufanya kazi kwa bidii na weledi ili kuleta matokeo Chanya katika shughuli za serikali na kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo mbalimbali katika kutekeleza majukumu ya kila siku.