Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

NAIBU WAZIRI MHE. QWARAY AWAAGIZA WAAJIRI KUTATUA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI KWA WAKATI


Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina  Qwaray, amewaagiza waajiri kuhakikisha changamoto na stahiki za watumishi wa umma zinashughulikiwa kwa wakati, hatua inayolenga kuongeza ufanisi na kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Qwaray ametoa agizo hilo leo Septemba 15, 2026  wakati akizungumza na watumishi wa umma wa Halmashauri ya Wilaya ya Buchosa mkoani Mwanza  kwa lengo la  kusikiliza changamoto za watumishi na kujadili namna ya kuboresha utendaji katika Utumishi wa Umma.

Amesema masuala yanayohusu kupandishwa vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao yanapaswa kushughulikiwa kwa wakati na mamlaka husika, badala ya kuendelea kucheleweshwa. "Nawaagiza waajiri wote kuhakikisha changamoto na stahiki za watumishi, ikiwemo kupandishwa vyeo, uhamisho, malimbikizo ya mishahara na mafao, zinashughulikiwa kwa wakati,” amesema  Mhe Qwaray.

Aidha, amesisitiza kuwa madai ya watumishi yanapaswa kuhakikiwa ipasavyo na kuwasilishwa yakiwa na nyaraka zote muhimu ili kuwezesha malipo kufanyika kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Mhe. Qwaray amezitaka Mamlaka za Ajira na Nidhamu kusimamia haki na wajibu wa watumishi kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na Taratibu za Utumishi wa Umma, huku akiwataka kuachana na utendaji wa mazoea. Amesema mambo yaliyo ndani ya mamlaka za waajiri na Mamlaka za Ajira na Nidhamu yanapaswa kushughulikiwa katika ngazi husika badala ya kuendelea kuwasilishwa Ofisini kwake.

Aidha, Mhe. Qwaray amesisitiza umuhimu wa watumishi kutumia mifumo ya kidijitali iliyobuniwa  na Serikali katika kusimamia utendaji na kupata huduma za kiutumishi. Mifumo hiyo ni pamoja na e-Watumishi, Watumishi Portal, e-Utendaji (PEPMIS) na e-Mrejesho, ambayo imeimarishwa kwa ajili ya kurahisisha upatikanaji wa huduma, kuongeza uwajibikaji na kutoa fursa kwa wananchi na watumishi kuwasilisha maoni, pongezi, malalamiko na mapendekezo.

Amesema matumizi sahihi ya mifumo hiyo ni sehemu ya jitihada za kujenga Utumishi wa Umma unaozingatia haki, wajibu, uwajibikaji, ufanisi na matumizi ya teknolojia.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Buchosa, Bw. Benson Mihayo amesema changamoto za watumishi zitaendelea kushughulikiwa kutokana na bajeti iliyopo huku akibainisha kuwa mwitikio wa watumishi katika suala  ujazaji PEPMIS limekuwa na mwitikio mkubwa ukilinganisha na hapo awali  hali inayopelekea malalamiko ya watumishi kupungua wakati wa upandaji wa madaraja.

Naye Mbunge wa Buchosa, Mhe. Erick Shigongo ametumia fursa hiyo kuwashukuru Watumishi wa Halmashauri ya Buchosa kwa huduma bora wanazoendelea kutoa kwa wananchi wa Halmashauri hiyo. " Hatua ya maendeleo unayoyaona leo hapa Buchosa ni kutokana na uwepo wa watumishi wazalendo waliojitoa kwa lengo la kuwahudumia wananchi" amesisitiza Mhe. Shigongo