Habari
NAIBU KATIBU MKUU LWANGILI AIPONGEZA MOI KWA KUENDESHA KLINIKI YA UPIMAJI AFYA, AAHIDI KUONGEZEKA KWA ARI YA UTENDAJI KAZI
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bi. Prisca Lwangili ameishukuru Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) kwa kuendesha zoezi la upimaji afya na huduma za matibabu kwa watumishi wa ofisi hiyo ambayo itasaidia uimara wa afya za watumishi hao na kuongeza ari ya utendaji kazi.
Bi. Lwangili ametoa rai hiyo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na Watumishi na Madaktari hao katika eneo maalum mara baada ya kuhitimisha rasmi zoezi la upimaji afya na matibabu kutoka kwa madaktari bingwa wa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI).
“Niwahakikishie mbegu mliyoipanda mtaivuna, mtaona matokeo ya uimara zaidi wa afya za watumishi wetu, wiki nzima tumeona watumishi wengi wakishiriki katika zoezi la upimaji afya na kupatiwa matibabu, tunaishukuru sana Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) tunaamini afya za watumishi hawa zitakuwa imara zaidi na itaongeza ari ya utendaji kazi,” amesema Bi. Lwangili
Aidha, Bi. Lwangili amewapongeza watumishi wa ofisi hiyo kwa kuwatumikia watumishi wa umma wenzao na wananchi waliofika kupata huduma katika ofisi hiyo pamoja na kwamba walikuwa katika zoezi la upimaji wa afya lakini huduma nyingine za kiutumishi ziliendelea kutekelezwa kwa wakati.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Musa Magufuli amesema Ofisi ya Rais-UTUMISHI itaendelea kufanya mazoezi ya mara kwa mara hasa kwa siku mbili Jumanne na Alhamisi ambazo zimepangwa maalum kufanyika kwa mazoezi hayo baada ya muda wa kazi.
Bw. Magufuli ameahidi kuwa watumishi wa ofisi hiyo watakuwa mabalozi wazuri kwa watumishi wengine kwa lengo la kuimarisha afya zao.
Naye, Daktari Bingwa wa Upasuaji-Magonjwa ya Ubongo, Uti wa Ubongo na Mishipa ya Fahamu kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), Bw. Hamisi Shabani ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa ushirikiano mkubwa ambao wameuonyesha wakati taasisi hiyo ilipokuwa ikitoa huduma za upimaji wa afya na matibabu.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu mkubwa sana kwa watumishi hao kuzingatia mazoezi na kupata mlo kamili utakaowafanya kuwa na afya bora na kuwajengea utimamu katika utekelezaji wa majukumu yao kwa ustawi wa Taifa.
Kwa wiki nzima Wataalam kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) walitoa huduma mbalimbali kwa watumishi wa ofisi hiyo ikiwemo huduma ya mifupa, mgongo, mishipa ya fahamu, magonjwa ya ndani mazoezi ya tiba na lishe pamoja na ushauri nasaha.
