Habari
MWIGULU ASISITIZA UMUHIMU WA KULINDA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, ametoa maagizo sita kwa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), akisisitiza umuhimu wa kulinda, kutunza na kutumia ipasavyo kumbukumbu na nyaraka kwa ajili ya kuhifadhi historia na urithi wa Taifa.
Dkt. Nchemba ameitaka TRAMPA kuhakikisha historia ya Taifa inalindwa, huku ikizingatia utoaji wa huduma bora kwa wananchi wanaohitaji huduma katika ofisi za umma.
Aidha, ameiagiza Taasisi za Umma kuanzisha vituo vya kisasa vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, sambamba na kuhimiza matumizi ya mfumo wa Ofisi Mtandao (e-Office) katika utekelezaji wa majukumu ya Serikali.
Ameitaka Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kufuatilia mara kwa mara matumizi ya mfumo wa e-Office na kubaini taasisi na ofisi ambazo hazitumii mfumo huo ili hatua stahiki zichukuliwe.
Vilevile, Dkt. Nchemba amezitaka Ofisi za Umma kuwekeza katika matumizi sahihi ya kumbukumbu na nyaraka, pamoja na kutathmini utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 katika maeneo yanayohusu menejimenti ya kumbukumbu na nyaraka.
Amesisitiza pia kuwa watendaji wa TRAMPA wanapaswa kunufaika na ongezeko la mshahara la mwaka (Annual Salary Increment), kwa kuzingatia taratibu na miongozo ya Serikali.
Maagizo hayo yamesomwa leo, Septemba 23, 2026, na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, wakati wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha Menejimenti ya Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), jijini Dodoma.
