Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MKOMI AZISHUKURU WIZARA, TAASISI KUFANIKISHA WIKI YA UTUMISHI WA UMMA


Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, amezishukuru Wizara na Taasisi za Umma kwa ushiriki wao katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yanayofanyika katika Viwanja vya Chinangali Park jijini Dodoma.

Bw. Mkomi alitoa shukrani hizo Juni 22, 2026 baada ya kutembelea mabanda ya maonesho ya taasisi mbalimbali zinazotoa huduma na elimu kwa wananchi wakati wa maadhimisho hayo, ambapo amepongeza juhudi zinazofanywa na washiriki katika kuwasogezea wananchi huduma muhimu za Serikali.

Amesema ushiriki mkubwa wa Wizara, Taasisi za Umma umechangia kufanikisha maadhimisho hayo kwa kuwawezesha wananchi kupata taarifa sahihi kuhusu huduma zinazotolewa na Serikali.

“Maadhimisho haya yamekuwa jukwaa muhimu la kuimarisha uhusiano kati ya Serikali na wananchi kwa kuwapatia huduma, elimu na kupokea maoni yao kuhusu namna ya kuboresha utoaji wa huduma za umma,” amesema Bw. Mkomi.

Aidha, amewataka watumishi wa umma kuendelea kuzingatia weledi, uwajibikaji na matumizi ya teknolojia katika utoaji wa huduma ili kuongeza ufanisi na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka 2026 yamewakutanisha Wizara na Taasisi za Serikali kwa lengo la kuonesha huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na kuhamasisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi.