Habari
MKOMI ATOA WITO KWA WATUMISHI KUJICHUNGUZA KAMA WANAFAA KUWA VIONGOZI
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Bw. Juma Mkomi amesema kuwa mtumishi wa umma anaweza kujifanyia uchunguzi (vetting) mwenyewe juu ya tabia na mwenendo katika utendaji kazi bila kusubiri taarifa ya vyombo vya usalama.
Bw. Mkomi alisema hayo Desemba 15, 2025 kwa Watumishi wa Ofisi hiyo wakati wa kuhitimisha mafunzo ya uelewa wa namna bora ya kulinda taswira nzuri ya taasisi yaliyofanyika Mtumba jijini Dodoma.
“Mtumishi anaweza kujichunguza na kuona kama anafaa kuwa kiongozi au la, kwa sababu tabia njema au mbaya anaweza kuitambua kwa ufasaha mtumishi mwenyewe” alisema Bw. Mkomi.
Bw. Mkomi aliongeza kuwa tabia na mienendo ya watumishi inatakiwa kuwa na taswira chanya kwao wenyewe na mbele ya macho ya wale wanaopokea huduma kutoka kwao.
Aidha, Bw. Mkomi alisisitiza kuwa tabia na mienendo ya watumishi wa ofisi hiyo inatakiwa kwenda sambamba na misingi mikuu ya utendaji kazi wa ofisi, pia tabia hizo zitoe mitazamo chanya juu ya utendaji kazi wao na namna anavyowahudumia watumishi wa umma na umma kwa jumla.
Awali, Mkufunzi Bw. Moses Raymond alisema kuwa Watumishi wa Ofisi ya Rais UTUMISHI ni kioo kwa watumishi wengine wote katika utumishi wa umma na ndio wenye dhamana ya kusimamia utumishi wa umma nchini. Hivyo, hawana budi kuwaongoza watumishi wengine vyema katika ujenzi wa taswira chanya ya Serikali.
Alifafanua kuwa, mtumishi wa Ofisi ya Rais UTUMISHI akifanya vibaya katika utoaji wa huduma, wananchi wanatafsiri kuwa watumishi wote wa ofisi hiyo wana tabia hiyo.
“Binafsi natoa rai katika mafunzo haya kuhakikisha kila mmoja anashiriki ipasavyo katika jitihada za ujenzi wa taswira nzuri ya ofisi kwa kufanya vyema hususani katika utekelezaji wa majukumu yake ili kulinda taswira chanya ya ofisi” aliongeza Bw. Raymond.
