Habari
MICHEZO YA SHIMIWI YA 40 MWAKA 2026 YAZINDULIWA RASMI - ZAWADI KWA WASHINDI KUBORESHWA 2027.
Michezo ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) ya 40 kwa mwaka 2026 imezinduliwa rasmi leo Jumamosi, Septemba 26, 2026, katika viwanja vya Chuo cha Mafunzo ya Polisi (CCP), Moshi, mkoani Kilimanjaro.
Uzinduzi huo umehudhuriwa na watumishi kutoka Wizara, Idara na Taasisi mbalimbali za Serikali, huku mgeni rasmi akiwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Christian Makonda (Mb). Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mhe. Makonda ameipongeza Kamati Tendaji ya SHIMIWI kwa kuhakikisha michezo hiyo inaendelea kufanyika kila mwaka, huku akisisitiza umuhimu wa kufanya maboresho zaidi katika michezo hiyo.
Mhe. Makonda amesema kuwa michezo hiyo kwa mwaka 2027 anatamani ifanyike mkoani Arusha huku akiahidi kufanya mapinduzi katika maandalizi, hususan eneo la zawadi kwa washindi, ikiwemo uwezekano wa kuwepo kwa zawadi za fedha taslimu.
Akihitimisha hotuba yake, Mhe. Makonda amesema: “Michezo si afya tu, michezo si uchumi tu, bali ni umoja wetu na ushirikiano wetu.”
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya SHIMIWI, Ndugu Daniel Mwalusamba akitoa salamu za Kamati pamoja na wanamichezo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutoa kibali na kuruhusu michezo hiyo kufanyika ikiwa ni pamoja na kuwawezesha watumishi kushiriki kikamilifu.
Ndugu Mwalusamba pia ameahidi kusimamia michezo hiyo kwa ufanisi na kuhakikisha watumishi waliofika mkoani Kilimanjaro wanashiriki ipasavyo, huku wakizingatia kanuni na taratibu za Utumishi wa Umma.
Michezo ya SHIMIWI kwa mwaka 2026 inafanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro, ambapo Ofisi ya Rais UTUMISHI ni miongoni mwa Wizara zinazoshiriki huku lengo la michezo hiyo likiwa ni kuwawezesha watumishi wa Serikali kukutana, kushirikiana na kujenga mahusiano mema, pamoja na kuimarisha afya, utimamu wa mwili na akili.
Michezo ya SHIMIWI ya mwaka 2026 inaongozwa na kaulimbiu isemayo “WATUMISHI WA UMMA TUPO TAYARI KWA AFCON 2027".
