Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. SIMBACHAWENE AITAKA OFISI YAKE KUTOA USHIRIKIANO WA KIUTENDAJI KWA NAIBU WAZIRI SANGU ILI KUBORESHA UTUMISHI WA UMMA NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ametoa wito kwa watumishi  pamoja na wakurugenzi wa Idara na Vitengo wa ofisi yake kutoa ushirikiano wa kiutendaji kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Deus Sangu aliyeteuliwa na kuapishwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kutumikia ofisi hiyo.

Mhe. Simbachawene ametoa wito huo leo jijini Dodoma, wakati wa hafla fupi ya kumpokea kiongozi huyo.

Mhe. Simbachawene amesema, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imepata kiongozi mwingine kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kiutendaji, hivyo ametoa rai kwa menejimenti ya ofisi hiyo kumpa ushirikiano wa kutosha ili aweze kutekeleza majukumu yake kikamilifu ili kufikia maono ya Rais wa Awamu ya Sita ya kuuboresha Utumishi wa Umma nchini.

“Tumepata kiongozi mwingine kwa ajili ya kuongeza nguvu ya kiutendaji, niwatake mtoe ushirikiano kwa Naibu Waziri Sangu ili kumuwezesha kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kutoa mchango katika Utumishi wa Umma kama ilivyokusudiwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan” amesema Mhe. Simbachawene.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa ofisi hiyo Mhe. Deus Sangu ameahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa watumishi wote na kuongeza kuwa, atahakikisha anasimamia haki katika kufanya kazi.

Mhe. Sangu ameongeza kuwa, ataendeleza pale alipoishia mtangulizi wake katika kuujenga utumishi wa umma wenye uadilifu na unaowajibika kwa wananchi katika kutoa huduma bora ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa malengo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ya kuujenga utumishi wa umma unaowajibika kwa wananchi.