Habari
MHE. SIMBACHAWENE AIELEKEZA TASAF KUOKOA MAISHA YA MAMA NA MTOTO KATIKA KIJIJI CHA BUNGU-KOROGWE

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. George Simbachawene ameuelekeza uongozi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kufanya tathmini ya ujenzi wa jengo la afya ya mama na mtoto katika Kijiji cha Bungu, Kata ya Bungu, Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga ili kuwaondolea adha ya upatikanaji wa huduma hiyo wakazi wa Kata hiyo.
Mhe. Simbachawene amesema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa maendeleo ya miradi ya TASAF katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga.
“Nimesikia katika maelezo yenu kuwa mna changamoto ya upatikanaji wa huduma za afya hususan ya mama na mtoto, nawaelekeza viongozi wa TASAF mfanye tathmini ya ujenzi wa jengo la huduma ya mama na mtoto ambalo litajumuisha huduma zote anazotakiwa kupata mama na mtoto,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Amesema, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akifanya kazi usiku na mchana kutafuta fedha kwa ajili ya kuwahudumia wananchi wake na hii ndio zawadi yake kubwa kwa wananchi, hivyo ni lazima wapatiwe huduma muhimu ikiwemo hiyo ya jengo la afya.
Aidha, Mhe. Simbachawene amewapongeza walengwa wa TASAF wa Kijiji hicho cha Bungu kwa kutumia vizuri ruzuku wanayoipata katika kufanya maendeleo.
“Nimefurahi sana kwa shuhuda mlizozitoa hapa, inaonesha ni jinsi gani mnavyotumia vizuri ruzuku ya TASAF mnayoipata, nina uhakika jambo hili hata Rais wetu mpendwa akilisikia litamfurahisha sana na kuwa na moyo wa kuendelea kutafuta fedha nyingine ili muendelee kunufaika,” Mhe. Simbachawene amesisitiza na kuwahimiza walengwa hao kuendelea kujishughulisha na masuala ya maendeleo ili wasirudi tena katika umasikini.
Vilevile Mhe. Simbachawene amewasisitiza walengwa hao pamoja na wananchi wa Kijiji cha Bungu kutunza miradi yote iliyoanzishwa katika kijiji hicho.
“Nimeshuhudia kisima cha maji na nimekunywa maji yake ambayo ni mazuri, rai yangu kwenu ni kukitunza ili kiwasaidie kwani ni suluhisho kubwa katika changamoto ya upatikananji wa maji,” Mhe. Simbachawene amesisitiza.
Mhe. Simbachawene ameendelea na ziara yake ya kikazi ya kuzungumza na watumishi wa umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF mkoani Tanga ambapo leo ametembelea Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe.