Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MHE. RIDHIWANI KIKWETE AISISITIZA e-GA KUHAKIKISHA DHANA YA MIFUMO KUSOMANA INAONEKANA DHAHIRI KWA WANANCHI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameisisitiza Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kuendelea kuunganisha mifumo ya Serikali kwenye Mfumo wa Kuwezesha Mifumo ya Serikali kuwasiliana na kubadilishana taarifa (Government Enterprise Service Bus (GovESB) ili dhana ya kusomana kwa mifumo hiyo ionekane kwa wananchi.

 

Akizungumza na Menejimenti na Watumishi wa Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) leo tarehe 25.11.2025, jijini Dodoma, Mhe. Kikwete ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kuanza utekelezaji wa maelekezo ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuunganisha mifumo hiyo kusomana na kusisitiza kuongeza kasi ya uunganishwaji wa mifumo ambayo bado haijaunganishwa.

“Ninawasisitiza Mifumo yote ambayo bado haijaunganishwa iunganishwe, dhana ya Mifumo kusomana ionekana dhahiri kwa wananchi na kutoa mfano kuwa mwananchi anapoenda kupata huduma akitoa namba yake ya NIDA taarifa zake zote za msingi zipatikane,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

 

“Wito wangu kwenu ni kuendelea kuongeza kasi ya mifumo kusomana ili kurahisisha utoaji wa huduma na kuwapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma kwani Serikali yetu inatakiwa kuwasiliana kidijiti,” Mhe. Kikwete amesisitiza.

 

Pia ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kuendelea kushirikiana na Taasisi za Umma kufanya uchambuzi, kusanifu na kujenga Mifumo mipya ya kieletroniki itakayosaidia kuboresha ufanisi katika utoaji wa huduma za Umma. “Ninawapongeza kwa kuendelea kusanifu na kujenga Mifumo mbalimbali ya TEHAMA Serikalini ambayo imeboresha utoaji wa huduma za Umma, haya ni mafanikio makubwa, kupunguza matumizi ya makaratasi,” Mhe. Kikwete ameongeza.

 

Aidha, Mhe. Kikwete ametoa wito kwa taasisi hiyo kutenga bajeti ya kutosha kwa ajili ya watumishi wake kujiendeleza ili kupata upeo mpana katika masuala ya teknolojia ambayo yanakuwa kwa kasi.

 

Kwa upande wake Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray, ameomba ushirikiano toka kwa Watendaji wa Taasisi hiyo.

“Ili tuweze kufanya kazi vizuri ni lazima tushirikiane, nitaendelea kuwa mwanafunzi wenu ili kazi ya Mamlaka hii ifanyike vizuri kwa ufasaha.” Mhe. Qwaray ameongeza

Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Mkurugenzi Mkuu wa eGA, Mhandisi Benedict Ndomba amesema Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 yenye jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.

Ameongeza kuwa e-GA inakusudia kutekeleza afua mbalimbali ili kusaidia taasisi za umma kutoa huduma mtandao kwa ufanisi.

Mhe. Kikwete ameendelea na ziara yake ya kikazi aliyoianza jana katika Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora akiambatana na Naibu Waziri wake Mhe. Regina Qwaray kwa lengo la kujitambulisha na kuboresha utendaji kazi.