Habari
MHE. KIKWETE ATOA WITO KWA WATUMISHI WA UMMA KUONGEZA KASI YA UWAJIBIKAJI ILI KUTOA HUDUMA BORA KWA WANANCHI
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Ridhiwani Kikwete amewataka watumishi wa Ofisi hiyo kuwa tayari kufanya kazi kwa kasi na kutoa huduma bora kwa wananchi.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa kampeni aliahidi mambo mengi na anatamani matokeo yaonekane kwa wananchi ndani ya muda mfupi, hivyo tunatakiwa kuongeza kasi na kukamilisha ahadi zake kwa wakati” alisema Mhe. Kikwete.
Waziri Kikwete aliyasema hayo alipokuwa akiongea na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Menejimenti ya Ofisi hiyo Novemba 18, 2025 wakati wa makabidhiano ya Ofisi hiyo Mtumba Jijini Dodoma.
Mhe. Ridhiwani amesema Serikali inaendelea kuboresha Utumishi wa Umma ili kumkomboa mwananchi na changamoto ya upatikanaji wa huduma bora.
Pia, Mhe. Kikwete amesema anatambua uhitaji mkubwa wa Watanzania hasa kwenye suala la ajira na kuelezea mkakati mkubwa utakaofanywa na Serikali katika kutatua changamoto ya ajira kwa Watanzania.
Kwa upande wake Naibu Waziri Mhe. Regina Qwaray amewasisitiza watumishi wa Ofisi hiyo kutoa ushirikiano kwa viongozi na watumishi wengine katika utendaji huku kila mmoja akitambua nafasi na thamani ya mwingine ili kufikia malengo ya Serikali ya utoaji wa huduma bora kwa ustawi wa taifa.
