Habari
MABADILIKO YA KIUTENDAJI YANAANZA NA MTUMISHI MWENYEWE - “Kaimu Katibu Mkuu UTUMISHI, Bi. Mavika”

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bi. Leila Mavika amesema mabadiliko ya kiutendaji kwa watumishi yanatakiwa kuanza na mtumishi mwenyewe kabla ya taasisi kutaka kufanya mabadiliko hayo.
“Mafunzo haya yanalenga kuwajengea uwezo ili mtekeleze majukumu yenu kwa ufanisi na kujiandaa kuwa viongozi bora wa baadae kwani ukishafikia hatua ya mtumishi mwandamizi basi unaweza kuwa kiongozi wakati wotewote.” Bi. Mavika ameongeza.
Bi. Mavika amesema taifa lolote ili lisonge mbela linahitaji kuwa na rasilimaliwatu yenye ujuzi, hivyo ameipongeza Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu ya Ofisi hiyo kwa kuandaa mafunzo hayo muhimu ya kuboresha utendaji kazi.
Amesema ni matarajio ya Menejimenti ya Ofisi hiyo kuona watumishi hao wanakuwa tofauti kiutendaji baada ya kupata mafunzo, hivyo aliwataka kuwa wasikivu na kufuatilia kwa umakini mada zinazotolewa na wawezeshaji.
“Wawezeshaji wetu ni wabobezi katika masuala ya utumishi wa umma, hivyo usikivu wenu utawasaidia kuboresha utendaji kazi wenu kama ambavyo Menejimenti inatarajia kwa maendeleo ya taifa letu.” Bi. Mavika amesisitiza.
Naye aliyekuwa Katibu Mkuu- Ofisi ya Rais - UTUMISHI ambaye ni mmoja wa wawezeshaji wa mafunzo hayo, Dkt. Larean Ndumbaro, ametoa wito kwa Maofisa hao kufanya kazi kwa umakini mkubwa hasa katika kushauri masuala mbalimbali.
“Ninyi mko kwenye Ofisi nyeti, hivyo mnapofanya kazi ni lazima kazi zenu ziendane na hadhi ya Ofisi, hasa pale mnapoa ushauri kwa Viongozi wenu, ushauri mtakaoutoa ni lazima uwe wa manufaa kwa taifa.” Dkt. Ndumbaro amesisitiza.
Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Musa Magufuli alisema jumla ya Maofisa Waandamizi 62 wa Ofisi hiyo wanashiriki mafunzo hayo yatakayofanyika kwa muda wa siku mbili.