Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

MAAFISA SHERIA NA RASILIMALIWATU WATAKIWA KUTUMIA SHERIA, KANUNI, TARATIBU NA MIONGOZO KATIKA KUSHUGHULIKIA MASUALA YA KIUTUMISHI


Na. Veronica Mwafisi-Dodoma

Tarehe 18 Machi, 2024

Kaimu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Xavier Daudi amewataka Maafisa Sheria na Maafisa Rasilimaliwatu kutambua kuwa kada zao ni za kimkakati kwa maendeleo ya Taifa.

“Rasilimaliwatu na Sheria vikisimamiwa vibaya vinaweza kuleta matokeo hasi katika utendaji kazi hivyo, kushusha uchumi na kusababisha taifa kushindwa kufikia malengo yake ya kutoa huduma bora kwa umma” amesisitiza Bw. Daudi.

Bw. Daudi ameyasema hayo leo tarehe 18 Machi, 2024 Jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kujadili changamoto za utekelezaji wa Sheria, Kanuni na Miongozo ya Utumishi wa Umma.

Ameongeza kuwa Sheria, Kanuni na Miongozo inayotumika sasa imetengenezwa na viongozi waliotangulia ambao walitamani kuona utumishi wa umma nchini unaendelea, hivyo Maafisa hao wametakiwa kuongeza ubunifu na kutenda haki katika utekelezaji wake.

Aidha Bw. Daudi amesema uzembe na kutokuwa na tabia ya kujisomea kumesababisha kuwa na changamoto ya ukiukwaji wa sheria, kanuni, miongozo ya kazi katika utumishi wa umma.

Akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Huduma za Sheria, Bi. Hilda Kabissa ameelezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kukumbushana kuhusu namna bora ya kutekeleza Sheria za Utumishi wa Umma na kanuni zake na kubadilishana uzoefu.

Bi. Hilda amebainisha kuwa, baadhi ya maafisa wa taasisi za umma wamekuwa wakiandika barua kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma wakiomba ufafanuzi wa masuala ya kawaida na ambayo yangeweza kutatuliwa katika maeneo yao kwa haraka, hivyo kikao hiki kitawajenga na kuwapa uelewa wa pamoja na namna bora ya kushughulikia masuala hayo ya kiutumishi mahala pa kazi.

Kikao kazi hicho kinafanyika kwa muda wa siku mbili tarehe 18 na 19 Machi, 2024 katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.