Habari
MAAFISA RASILIMALIWATU WATAKIWA KUFANYA TATHMINI KWENYE SUALA LA UHAMISHO KWA WATUMISHI WA UMMA
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw, Juma Mkomi ametoa wito kwa Maafisa Rasilimaliwatu kufanya tathmini kwenye suala la uhamisho kwa watumishi wa umma ili kuondoa vikwazo na kuongeza tija ya utendajikazi katika Utumishi wa Umma.
Bw. Mkomi ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifunga mafunzo ya Mfumo wa e-Watumishi kwa Maafisa Rasilimaliwatu na Maafisa Tawala kutoka Taasisi mbalimbali za Umma yaliyokuwa yakifanyika kwa siku tisa kuanzia tarehe 23 Machi hadi 01 Aprili, 2026 jijini Dodoma.
Bw. Mkomi amesema, uhamisho ni haki ya mtumishi na mwajiri kutaka kumtumia mtumishi fulani katika eneo fulani au ni haki ya mwajiri kuendelea kumtumia mtumishi husika sehemu anayotumikia vizuri.
Hivyo, Bw. Mkomi amewataka Maafisa Rasilimaliwatu hao kufanya tathmini katika maeneo yao ya kazi hasa katika Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma (e-Msawazo).
“Nitoe msisitizo kuhusu tathmini ya mahitaji ya rasilimaliwatu, naamini ninyi ndio wasimamizi wakubwa katika maeneo mengi na ndio mnaoleta taarifa ya masuala husika ya kiutumishi, utaratibu wa uhamisho una vigezo na vinajulikana hivyo ni vema kupata usahihi wa taarifa za watumishi au mahitaji ya watumishi hao pasipo kuwa na vikwazo au mifarakano isiyokuwa na tija kwa sababu ya uhamisho,” amesisitiza Bw. Mkomi.
Aidha, Bw. Mkomi ameongeza kuwa, Maafisa Rasilimaliwatu wana jukumu la kumshauri vizuri mwajiri linapotokea suala la uhamisho kwa mtumishi ni vema kutoa vigezo sahihi baada ya kufanya tathmini ya kutosha.
“Tunatamani umwambie mwajiri uhamishio wa mtumishi huyu tusiutekeleze kwa sababu tathmini tuliyoifanya ya rasilimaliwatu katika eneo letu tuna upungufu wa afisa husika au uhamisho huu tuutekeleze kwa sababu tuna maafisa wa kutosha kadhaa kwenye eneo letu,” amesema Bw, Mkomi
Kadhalika, Bw. Mkomi amesema eneo la uhamisho limeonekana kuwa na changamoto kutokana na watumishi wanaoomba uhamisho kuzuiliwa bila kuwa na sababu za kutosha.
Bw. Mkomi amewataka Maafisa hao kufanyia kazi mafunzo yote waliyoyapata watakaporudi kwenye maeneo yao ya kazi ili yakaongeze tija katika Utumishi wa Umma
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Rasilimaliwatu Serikalini, Bw. Hamis Mkunga amesema jumla ya washiriki 275 wamepatiwa mafunzo hayo hivyo amewataka washiriki hao kwenda kufanyia kazi ili kuleta matokeo chanya katika maeneo yao ya kazi kwa maendeleo ya ofisi au taasisi husika na taifa kwa ujumla.
Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Mafunzo hayo, Bi. Isabela Chilumba amemuahidi Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais-UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi kuwa kwa niaba ya washiriki wote watazingatia maelekezo ambayo ameyatoa ili waweze kuboresha utendaji kazi kwa ustawi wa Taifa.
