Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU MKOMI AWATAKA WADAU WA RASILIMALIWATU KATIKA SEKTA YA UMMA KUPENDEKEZA MKAKATI MADHUBUTI WA SULUHISHO LA UPUNGUFU WA WATUMISHI


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw, Juma Mkomi amewataka wadau wa Rasilimaliwatu Serikalini kupendekeza mkakati madhubuti utakaosaidia kuepukana na changamoto ya upungufu wa watumishi katika taasisi za umma.

Katibu Mkuu Mkomi ameyasema hayo leo jijini Dodoma alipokuwa akifungua kikao kazi cha Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka katika Wizara na Taasisi za Kimkakati kilicholenga kujadili matokeo ya tathmini ya mahitaji ya rasilimaliwatu.

Amesema Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ilifanya zoezi la Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika taasisi za umma na kubaini kuwepo kwa upungufu wa watumishi kwenye baadhi ya taasisi na taasisi nyingine kuwepo kwa ziada ya watumishi.

Amesema kufuatia tathmni hiyo, Ofisi iliona ni vema ikaandaa kikao cha wadau hao ili kujadiliana kwa pamoja namna itakavyofaa kutafuta ufumbuzi wa changamoto hiyo ya muda mrefu.

Amesema kila mwaka wakati wa bajeti taasisi za umma zimekuwa na utaratibu wa kuomba watumishi, hivyo mkakati madhubuti uwekwe ili kupata suluhisho la changamoto hiyo ya upungufu wa watumishi.

“Lengo kubwa la kikao kazi hiki ni kupata usahihi wa taarifa za watumishi au mahitaji ya watumishi katika taasisi za umma, kuna maeneo yanahitaji watumishi kimkakati hivyo ni muhimu kuona namna ya kukubaliana katika kuwapata watumishi hao na kujadiliana kwa kina ili kupata mapendekezo yatakayosaidia kuwagawa Watumishi wa ajira mpya na watakaokuwa wakihamia katika vituo vingine vya kazi,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda amesema kupitia kikao kazi hicho Serikali itapata taarifa zilizo sahihi  za mahitaji ya Watumishi wa Umma kwa miaka mitano ijayo.

Akitoa neno la shukrani Mwenyekiti wa Kikao kazi hicho ambaye ni Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu Wizara ya Afya, Bw. Issa Ng’imba alimuahidi Katibu Mkuu Mkomi kuwa watazingatia maelekezo yote ambayo ameyatoa ili waweze kuboresha utendaji kazi kwa maendeleo ya Taifa