Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KATIBU MKUU MKOMI AWATAKA WADAU KUTOA MAONI KATIKA MFUMO WA TATHMINI YA MAHITAJI YA RASILIMALIWATU ILI KUBORESHA UTENDAJI KATIKA UTUMISHI WA UMMA


Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amesema Mfumo wa Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu utaisaidia Serikali kufanya msawazo katika Utumishi wa Umma ili kuwa na mtawanyo mzuri wa watumishi kwa lengo la kuboresha utendaji katika utumishi wa umma.

Bw. Mkomi ameyasema hayo leo jijini Dodoma wakati akifungua kikao kazi cha kujadili matokeo ya tathmini ya mahitaji ya rasilimaliwatu katika utumishi wa umma kwa Wakurugenzi wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu kutoka Wizara zote, wataalamu wanaosimamia uandaaji na ujazaji wa mahitaji ya watumishi kutoka wizara zote pamoja na Wakurugenzi na wataalamu kutoka Ofisi ya Rais-UTUMISHI.

Bw. Mkomi amesema kila Mkurugenzi anafahamu umuhimu wa mahitaji ya rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma na kuwasihi wafanye tathmini ya kutosha.

“Ukisema una watumishi wachache, tutakuuliza unahitaji watumishi wangapi? kwani unatakiwa uwe umefanya tathmini ya kutosha kwasababu inawezekana kumhitaji kwako mtumishi au kutokumhitaji kunatokana na matakwa yako na si mfumo unaokufahamisha kuwa mtumishi huyu ni wa ziada.” Bw. Mkomi amesema.

Bw. Mkomi amesema msawazo katika utumishi wa umma unahitajika kufanywa katika maeneo mawili ikiwemo mjini ili kutokuwa na watumishi wa ziada ambao hawana majukumu ya kutosha katika maeneo yao ya kazi lakini pia msawazo huo utasaidia kuunganisha familia.

Bw. Mkomi ameongeza kuwa, msawazo hautaweza kufanyika bila kuwa na taarifa halisi ya mahitaji na idadi ya watumishi waliopo katika maeneo husika hivyo, ni vizuri washiriki wakaangalia namna ya kufanya kwani inatakiwa kujua watumishi wangapi wanahitajika wapi, wakafanye nini na baada ya kujua hayo itapatikana nafasi nzuri ya kuboresha. 

“Niwatake mshiriki kikamilifu kwa kuipokea taarifa hiyo, kuichambua na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuboresha Mfumo huo utakaowezesha kuwa na mtawanyo mzuri wa watumishi katika Taasisi za Umma.” Bw. Mkomi amesisitiza.

Akitoa neno la utangulizi, Mkurugenzi wa Uendelezaji Taasisi, Bw. Nolasco Kipanda ameelezea lengo la kikao kazi hicho kuwa ni kujadili matokeo ya tathmini ya Rasilimaliwatu katika Taasisi za Umma ili kupata maoni toka kwa wadau hao na kuboresha mfumo huo katika Utumishi wa Umma kwa masilahi mapana ya taifa.  

Kikao kazi hicho kilichoanza leo kinafanyika kwa muda wa siku mbili ambapo mada mbalimbali zitawasilishwa ikiwemo Matokeo ya Tathmini ya Mahitaji ya Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma, matokeo ya Wizara na vigezo kwa upande wa Wizara na Makundi ya Taasisi.