Habari
KATIBU MKUU MKOMI ATOA WITO WA KUPIMA AFYA ILI KUONGEZA TIJA, UFANISI NA UWAJIBIKAJI MAHALI PA KAZI
Na. Veronica Mwafisi-Dodoma
Tarehe 21 Septemba, 2026.
Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi ametoa wito kwa Watumishi wa Umma kupima afya zao mara kwa mara ili kujijua na kuona namna bora ya kuishi kwa lengo la kuongeza tija, ufanisi na uwajibikaji mahali pa kazi kwa maslahi mapana ya nchi.
Bw. Mkomi ametoa wito huo leo jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa ofisi hiyo katika eneo maalum la mafunzo mara baada ya madaktari kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), kutoa mafunzo kuhusu umuhimu wa lishe bora na namna bora ya kufanya mazoezi.
“Kupima afya mara kwa mara kunasaidia kujikinga na mambo mengi ikiwemo kubadilisha mtindo wa maisha, hivyo ni muhimu Watumishi wa Umma tukajenga utamaduni wa kuangalia afya zetu bila kulazimishwa,” amesisitiza Katibu Mkuu Mkomi.
Aidha, Katibu Mkuu Mkomi amewahimiza watumishi hao kwenda kwa wakati katika maeneo maalum ya ofisi hiyo yaliyotengwa kwa ajili ya kupima afya na kutoa ushirikiano kwa wataalam wa Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI) waliofika kutoa huduma hiyo.
Awali, Daktari kutoka Taasisi ya Tiba na Mifupa Muhimbili (MOI), Bw. Mkubwa Suleiman alisema ni muhimu watumishi hao wakazingatia mazoezi na mlo kamili utakaowafanya kuwa na afya bora ambayo ni nguzo muhimu kwa kila mtu.
Kwa upande wake, Daktari Adam Hussein pia kutoka katika Taasisi hiyo alisema, Watumishi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora wana majukumu mengi ikiwemo utoaji wa huduma mbalimbali za kiutumishi hivyo, ni muhimu kila mtumishi akajua afya yake ili waweze kutoa huduma bora kwa Wananchi wakiwa na utimamu wa afya.
Wataalam hao wamelenga kutoa huduma mbalimbali kwa watumishi wa ofisi hiyo ikiwemo huduma ya mifupa, mgongo, mishipa ya fahamu, magonjwa ya ndani pamoja na mazoezi ya tiba na lishe.
