Habari
KATIBU MKUU MKOMI ASISITIZA DHANA YA URITHISHANAJI MADARAKA KWA WATUMISHI WA UMMA NCHINI

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, UTUMISHI, Bw. Juma Mkomi ameitaka Idara ya Uendelezaji Rasilimaliwatu katika Ofisi hiyo kuongeza nguvu katika eneo la mafunzo ya umuhimu wa Urithishanaji wa madaraka kwa Watumishi wa Umma huku akiwataka Wakurugenzi na Wakuu wa Taasisi nchini kuwaandaa watumishi wao ili waweze kuwa viongozi wazuri hapo baadaye
Amesema Kiongozi mzuri ni yule anayewaandaa watumishi walio chini yake kuwa viongozi wazuri katika siku za usoni huku akionya dhana potofu iliyojengeka kuwa ukiwaandaa watumishi walio chini yako wataichukua nafasi uliyonayo
Amesema Serikali ina Taasisi nyingi ambazo zinahitaji watumishi hao walioandaliwa vizuri na kwa muda mrefu
Bw. Mkomi ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Agosti 18, 2025 katika ofisi hiyo iliyopo Mji wa Serikali Mtumba, jijini Dodoma wakati akizungumza na watumishi wa Ofisi hiyo mara baada ya kutolewa kwa mafunzo ya Uongozi, ikiwa ni muendelezo wa mafunzo hayo ambayo hutolewa kila wiki kwa Watumishi kwa lengo la kuboresha utendaji kazi wao
Amesema endapo kutakuwa na utamaduni huo wa kurithishana madaraka, watumishi watakaoandaliwa wataenda kuwa viongozi mahali pengine na sio lazima wabaki hapo hapo.
Awali Mwezeshaji wa Mafunzo hayo ya Uongozi, Dkt. Ntangeki Nshala amesema Uongozi sio lazima uwe unawaongoza watu bali ni kuonesha uwezo ulionao katika eneo ulilopo
Amesema uongozi ni suala binafsi na msukumo uliopo ndani ya mtu ndio maana uongozi unatofautiana katika ya mtu na mtu
Amesema uongozi ni kuonesha njia,kujaribu na kujiamini katika kufanya maamuzi popote ulipo na sio lazima uwe na cheo fulani
Aidha Dkt. Nshala amesema Watumishi wanahitaji kuwa na ujasiri na ndoto kubwa ya kufanya chochote wanachohitaji huku akionya tabia ya watu wengi ya kushindwa kuonesha uwezo wao kwa kisingizio cha uroho wa madaraka
Amesema Watumishi waliowengi mara baada ya kuajiriwa husahau kusudi la ndoto zao na hivyo hujikuta wakiishi ili mradi kwa sababu hali zao za kiuchumi huwa zimeimarika kidogo
" Ukiwa huna ujasiri huwezi kufanya mambo makubwa na hivyo wengi hujikuta wakijidumaza" amesisitiza Dkt. Nshala
Kufuatia hatua hiyo, Dkt. Nshala amesisitiza watumishi kujitambua na kuwa na dira na maono ya kutaka kuwa nani katika kazi na kwenye jamii kwa ujumla