Habari
KATIBU MKUU MKOMI APOKEA MAKOMBE YA USHINDI MASHINDANO YA SHIMIWI 2025 ASISITIZA UMUHIMU WA MICHEZO KWA WATUMISHI WA UMMA

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi, Septemba 24, 2025 amepokea makombe ya ushindi yaliyonyakuliwa na timu ya OfisI yake katika Mashindano ya Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) 2025, yaliyofanyika jijini Mwanza huku akisisitiza umuhimu wa michezo kwa Watumishi wa Umma nchini.
Akizungumza katika hafla fupi iliyofanyika sehemu ya wazi ya Ofisi hiyo, Katibu Mkuu Bw. Mkomi amezipongeza timu zote zilizoshiriki katika mashindano hayo ya SHIMIWI jijini Mwanza kwa juhudi na uzalendo waliouonesha hadi kuibuka mabingwa katika michezo mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu (wanaume) mabingwa nafasi ya kwanza, netiboli (wanawake) nafasi ya tatu, mbio za baiskeli na mchezo wa “darts” walipata ushindi wa nafasi ya tatu wa jumla, aidha kwenye mbio za kupokezana mita 400 (Relay) wanawake waliibuka mshindi wa kwanza na wanaume mshindi wa pili.
Bw. Mkomi amesema ushindi huo ni ishara ya mshikamano, nidhamu na mazoezi ya muda mrefu ya timu nzima. Amesisitiza kuwa michezo si tu burudani, bali pia ni nyenzo muhimu ya kuimarisha afya, mahusiano kazini na kuongeza ufanisi wa kazi.
“Michezo ni afya, hivyo ninawahimiza Watumishi wa Umma msiache kushiriki michezo kwani afya zenu zikiwa nzuri basi huduma zitatolewa kikamilifu kwa wananchi.” Amesisitiza na kuongeza kuwa pamoja na kuimarisha afya, pia inaleta ushirikiano.
Amesema Ofisi yake imeweka utaratibu wa watumishi kufanya mazoezi kila siku ya Jumanne na Alhamisi, hivyo amewasisitiza watumishi hao kushiriki kikamilifu.
“Utaratibu wa kufanya mazoezi kila Jumanne na Alhamisi tumeuweka makusudi ili kila mmoja ashiriki, hivyo ukifika muda uliopangwa wa kuanza mazoezi wote tunatakiwa kuelekea kwenye mazoezi,” ameongeza.
Pamoja na kuhimiza kushiriki michezo, Katibu Mkuu Mkomi amewataka Watumishi wa Umma kujiepusha na tabia zinazoharibu taswira ya Ofisi. “Haipendezi kuona mtumishi wa umma anafanya mambo ya ajabu huko mtaani, sisi ni kioo, hivyo tunatakiwa kuwa mfano wa kuigwa katika kuzingatia maadili ndani na nje ya ofisi," amesema.
Naye Mwenyekiti wa michezo wa timu ya UTUMISHI ambaye ni Afisa Tawala Mwandamizi wa Ofisi hiyo, Bw. Charles Shija kwa niaba ya wanamichezo wote, alimshukuru Katibu Mkuu kwa kuwawezesha kushiriki michezo hiyo na kupata ushindi.
Aidha, Bw. Shija pamoja na wanamichezo hao walitumia fursa hiyo kumkabidhi Katibu Mkuu makombe hayo huku wakiahidi kuendelea kujiimarisha zaidi katika michezo kwa ustawi wa taifa.