Habari
KATIBU MKUU MKOMI AKAGUA MAENDELEO YA MRADI WA UJENZI WA MAKAZI YA WATUMISHI KIJIJI CHA KIJIWENI

Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Bw. Juma Mkomi amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa makazi ya Watumishi wa Umma unaojengwa katika Kijiji cha Kijiweni, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi ili kuwasaidia watumishi hao kuwa karibu na ofisi wanazofanyia kazi kwa lengo la kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Akizungumza mara baada ya kukagua mradi huo leo, Katibu Mkuu Mkomi amesema ujenzi wa makazi ya watumishi hao utawasaidia kuepeukana na changamoto ya makazi ambayo imekuwa ikiwakabili na kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Amesema Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikiwajali sana watumishi wa umma katika kuboresha mazingira ya kazi ikiwemo utekelezaji wa mradi wa makazi ya watumishi.
“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutekeleza kwa vitendo azma yake ya kuujenga utumishi wa umma pamoja na kuboresha mazingira ya utendaji kazi wa watumishi wa umma ili wawe na tija katika utoaji wa huduma kwa maendeleo ya taifa,” Katibu Mkuu Mkomi ameongeza.
Bw. Mkomi amesema mradi wa ujenzi wa makazi hayo ya watumishi upo katika hatua ya majaribio katika Manispaa ya Lindi, mkoa wa Lindi ambapo pia unatekelezwa katika Mikoa ya Dodoma, Singida na Ruvuma.
Katibu Mkuu Mkomi katika ziara hiyo aliambatana na baadhi ya Wakurugenzi wa ofisi yake ambapo kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini, Bw. Patrick Allute amesema Watumishi Housing Investments ndiyo kandarasi inayojenga makazi katika mradi huo.
Bw. Allute ameongeza kuwa, mradi huo unafuatiliwa na kusimamiwa kikamilifu ili uweze kukamilika kwa wakati.