Habari
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YAMPONGEZA RAIS MHE. DKT. SAMIA SULUHU HASSAN KWA KUWEKA KIPAUMBELE KWENYE SUALA LA AJIRA
Kamati ya kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kulipa kipaumbele suala la ajira katika utumishi wa umma.
Pongezi hizo zimetolewa leo Machi 24, 2026 na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Edwin Swalle wakati akimwakilisha Mwenyekiti wa Kamati hiyo katika kikao cha kupokea Utekelezaji wa Bajeti ya Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa Mwaka wa Fedha 2025/26 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2026/27 kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Bunge jijini Dodoma .
Amesema kasi ya kutoa vibali vya ajira kwa sasa imekuwa ni kubwa na ya kuridhisha ukilinganisha na miaka iliyopita. “Kwa niaba ya Kamati nipende kutoa pongezi nyingi kwa Mhe. Rais kwa kutoa vibali vya ajira pamoja na wewe Mhe. Waziri Kikwete na wasaidizi wote kwa utekelezaji kwani tumeona msukumo mkubwa kwenye suala la ajira katika Serikali hii ya Awamu ya Sita, hongereni sana,” ameongeza Mhe. Swalle.
Aidha, amewapongeza Viongozi wa Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa ushirikiano kwa kamati hiyo ambao umerahisisha utekelezaji wa majukumu ya kamati.
“Mhe. Waziri Kikwete umekuwa ukitupatia ushirikiano mkubwa sana katika utekelezaji wa majukumu yetu, wewe pamoja watendaji wote wa Ofisi hii, mmefanya kazi yetu kuwa rahisi sana, hata katika ziara ya kamati tuliyoifanya Kanda ya Ziwa hivi karibuni hukuwahi kutuacha, ulikuwa nasi bega kwa bega, tunakupongeza kwa kuonyesha uko makini sana na kazi yako,” ameongeza Mhe. Swalle.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete amesema, Ofisi yake ipo tayari kutoa ushirikiano wowote unaohitajika katika kufanikisha utekelekezaji wa majukumu ya kamati ili kuweza kufikia malengo iliyojiwekea katika kuhudumia wananchi.
