Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora

Habari

KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAIPONGEZA OFISI YA RAIS UTUMISHI NA TAASISI ZAKE KWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KIKAMILIFU


Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora pamoja na taasisi zake kwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu na kuhakikisha huduma bora inatolewa kwa wananchi kwa wakati sahihi.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Joseph Mhagama ametoa pongezi hizo leo jijini Dodoma kwa niaba ya kamati yake wakati wa kikao kazi cha kamati hiyo na Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kilicholenga kupokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi ya mwezi Aprili hadi Septemba 2024.

“Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora imesheheni wabobezi wa sekta zote jambo linalowafanya watendaji wa ofisi hii pamoja na taasisi zilizopo chini yake kutekeleza majukumu yake kikamilifu.” Mhe. Dkt. Mhagama amesema.

Aidha Dkt. Mhagama ameishukuru Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kwa kutoa ushirikiano mkubwa kwa kamati hiyo kwani wajumbe wake wamekuwa wakipatiwa uelewa mpana juu ya utekelezaji wa majukumu ya kila taasisi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Dkt. Mhagama ameishauri Ofisi ya Rais- UTUMISHI na Utawala Bora kutoa mrejesho mara kwa mara kwa wananchi juu ya hatua mbalimbali ambazo imekuwa ikizichukua na kuzifanyia kazi baada ya kupokea malalamiko au changamoto ya masuala mbalimbali ili kuonesha namna ambavyo ofisi hiyo imekuwa ikiwajibika na kutekeleza majukumu yake kwa kiwango kikubwa.

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria itapokea na kujadili taarifa ya utendaji kazi wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Utawala Bora kwa siku mbili, tarehe 21 na 22 Oktoba, 2024.