Habari
KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA UTAWALA, KATIBA NA SHERIA YAIELEKEZA SEKRETARIETI YA MAADILI YA VIONGOZI WA UMMA KUTOA HUDUMA KIDIJITI
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria imepokea taarifa ya utendaji wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ambapo imeielekeza Taasisi hiyo kujikita zaidi kidijiti katika utoaji wa huduma mbalimbali kuhusu namna Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyofanya kazi jambo ambalo litawasaidia Viongozi wanaowajibika chini ya Sheria ya Maadili kuhusu Ujazaji wa Fomu za Tamko la Rasilimali na Madeni pamoja na Hati ya Ahadi ya Uadilifu kwa Viongozi wa Umma na Uwajibikaji wa pamoja ili waweze kukamilisha kwa wakati taarifa zitakazohitajika katika ujazaji wa fomu hizo.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo jijini Dodoma alipokuwa akihitimisha kikao cha Kamati yake na Watendaji wa Ofisi ya Rais-UTUMISHI na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma kilichokuwa na lengo la kupokea taarifa ya Utendaji wa Taasisi hiyo kuhusu usimamizi na ushughulikiaji wa maadili ya Viongozi wa Umma ikiwemo uhakiki wa uzingatiaji wa ahadi za uadilifu, tamko la mali na madeni na ushughulikiaji wa malalamiko na mashauri.
Mhe. Dkt Ndumbaro pia amesisitiza suala la kuongeza juhudi za kutoa elimu zaidi ya namna ya kujaza fomu mbalimbali za Maadili kwa Viongozi ili kuepukana na changamoto ya kuchelewesha ujazaji wa taarifa kwani, kuna baadhi ya Viongozi wanakuwa wapya katika uongozi hivyo inawalazimu kupewa uelewa mpana utakaowaongoza katika ujazaji wa fomu hizo.
Ameongeza kuwa, utoaji wa elimu zaidi utasaidia jamii kuona namna Taasisi hiyo inavyofanya kazi kubwa kwa maendeleo ya nchi.
“Ni vema kuongeza elimu zaidi kuhusu ujazaji wa fomu za maadili kwa Viongozi wanaowajibika chini ya sheria ili kuepukana na changamoto mbalimbali, wakati mwingine tunapata Viongozi wapya ambao hawana uelewa mpana juu ya ujazaji wa fomu hizo, hivyo elimu itakapotolewa itasaidia kupunguza changamoto hizo na kujaza kwa wakati fomu husika lakini pia elimu hiyo itawapa wananchi uelewa zaidi wa namna Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma inavyotekeleza majukumu yake kwa ufanisi,’’ Amesema Mhe. Dkt. Ndumbaro
Akiwasilisha taarifa hiyo, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, Naibu Waziri wa ofisi hiyo, Mhe. Regina Qwaray amesema Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ina jukumu la kusimamia tabia na mienendo ya Viongozi wa Umma ili kukidhi matakwa ya Sheria ya Maadili.
Mhe. Qwaray amesema, Majukumu ya Msingi ya Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma ni pamoja na kupokea na kufanya uhakiki wa Matamko ya Viongozi wa Umma kuhusu Rasilimali, kufanya utafiti juu ya hali ya Maadili na kushauri na kuweka mikakati katika masuala yanayohusu Uadilifu nchini, kufanya uchunguzi kuhusu ukiukwaji wa maadili yaliyotajwa na Sheria, kupokea na kushughulikia malalamiko na taarifa za ukiukwaji wa Maadili kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma kutoka kwa wananchi pamoja na kutoa elimu ya Maadili kwa Viongozi wa Umma.
Naibu Waziri Qwaray ameongeza kuwa, Katika kipindi cha Julai 2025 hadi Juni 2026, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma imetekeleza kazi za usimamizi na ushughulikiaji wa maadili ya viongozi wa umma ikiwemo uhakiki wa uzingatiaji wa ahadi za uadilifu, tamko la mali na madeni na ushughulikiaji wa malalamiko na mashauri pamoja na kusaini hati husika pindi viongozi wanapoteuliwa, kuajiriwa au kuchaguliwa
Pia Mhe. Qwaray amesema, elimu ya maadili itaendelea kutolewa katika shule na vyuo kupitia klabu za maadili ili kuweza kujenga na kuimarisha maadili ya kitaifa na kuyafanya yawe sehemu ya jamii pamoja na kuzuia mmomonyoko wa maadili nchini pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu Sheria ya Ulinzi wa watoa taarifa ambayo inamhakikishia usalama na ulinzi.
Akitoa neno la shukrani kwa Kamati hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ameishukuru Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria kwa kuendelea kutoa miongozo na maelekezo ya kiutendaji ambayo yanaongeza chachu na ufanisi katika kuboresha na kuimarisha utendaji kazi na kuleta tija katika kuwahudumia Viongozi na Wananchi kwa lengo la kujenga na kuimarisha Utawala Bora nchini.
