Habari
“IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA NI KIUNGO MUHIMU KATIKA HISTORIA YA NCHI YETU”- Mhe. Ridhiwani Kikwete
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete ametoa wito kwa Menejimenti na Watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kuendelea kukusanya taarifa, kumbukumbu, nyaraka na machapisho mbalimbali yanayohusu historia ya nchi yetu na waasisi wa Taifa letu ili kutoa taswira ya nchi yetu kwa vizazi vijavyo.
Mhe. Kikwete ametoa wito huo akiwa kwenye mwendelezo wa ziara ya kikazi katika taasisi zilizo chini ya Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambapo leo ametembelea katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
“Niwapongeze kwa kazi nzuri mnayofanya ya kukusanya kumbukumbu na nyaraka, ninyi ni kiungo muhimu sana katika historia ya nchi yetu, tuna kazi kubwa ya kutunza kumbukumbu na kuweka nyaraka sawa. Historia ya Tanzania yetu iko chini ya Idara hii, jambo kubwa na la msingi ni kuhakikisha kazi hii inafanyika kwa ufanisi. Mimi na mwenzangu Naibu Waziri pamoja na watendaji wa Ofisi yetu tuko tayari kuwapa ushirikiano, ili tutekeleze vizuri majukumu yaliyoainishwa katika muundo wa taasisi hii,” ameongeza Mhe. Kikwete.
Mhe. Kikwete pia ameielekeza Idara hiyo kuweka na kuhuisha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu (Keyword filling system and e-file management system) katika Taasisi za Umma ili kuongeza ufanisi na tija katika utoaji wa huduma Serikalini kwa kuwa suala hilo bado ni changamoto kubwa katika Taasisi nyingi za Umma.
Aidha, amewasisitiza kuendelea kutambua, kukusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu na vitu vya waasisi wa Taifa letu, kuendelea kuimarisha masijala katika Taasisi za Umma kwa kuzijengea uwezo Taasisi za Serikali kuhusu utunzaji wa kumbukumbu, kusimamia matumizi ya Mfumo wa e-Office na kuhakisha Roll Out ya Mfumo huo katika Taasisi zote za Umma pamoja na kusimamia maadili na taratibu za kiutendaji ili kukomesha vitendo vya uvujishaji wa Siri za Serikali;
Akitoa neno la utangulizi kabla ya kumkaribisha Mhe. Ridhiwani kuzungumza na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Regina Qwaray ameipongeza Ofisi hiyo kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kutunza kumbukumbu na nyaraka za taifa.
“Nimejifunza mambo mengi, nimepata darasa la kutosha sikujua kama kuna mambo mengi hapa kabla ya sisi kuzaliwa,” Mhe. Qwaray ameongeza
Ametoa wito kwa Menejimenti na Watumishi wa Idara hiyo kutangaza utekelezaji wa majukumu ya taasisi yao ili watu wengi hasa vijana wa Tanzania wakajifunze na kujua historia ya nchi yao na kuwa wazalendo.
