|
Kama sehemu ya kuelimisha kuhusu huduma zinazotolewa na serikali, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma (OR MUU) iliratibu Wiki ya Utumishi wa Umma kuanzia 16-23 Juni 2009, Pia ilishiriki maonesho ya kimataifa ya Saba Saba katika viwanja vya Mwalimu Julius K. Nyerere-Barabara ya Kilwa na Nane nane katika viwanja vya Nzuguni mkoani Dodoma 2009. yafuatayo ni maswali yaliyoulizwa na wadau mbalimbali, na majibu yake
Swali/Maoni: Nawapongeza kwa kazi nzuri. Hata hivyo kuna mengi ya kujifunza na kufanya ili kila mara muwe na mambo tofauti ili msiwachoshe watu waliowatembelea banda hili. Hongera kwa kuleta mashine ya kuweza kuangalia kumbukumbu za zamani Jibu: Tunashukuru kwa dhati kwa pongezi ulizozitoa. Ni kweli kuna umuhimu wa kuwa na mabadiliko ya vitu tunavyopeleka katika maonesho kila mwaka ili tusiwachoshe wateja wanaotutembelea. Aidha, tunakushukuru kwa ushauri na tunaahidi kuufanyia kazi na matokeo yataonekana katika maonyesho yanayokuja. Tutorial Assistant – TPSC. Swali/Maoni: Katika kada ya utunzaji kumbukumbu tunahitaji ushirikiano wa dhati zaidi katika Idara ya Utunzaji Kumbukumbu ili kuepusha ile dhana ya watunzaji Kumbukumbu kudharauliwa, wathaminiwe na kupewa motisha ili waweze kupenda kazi zao. Utumishi simamieni kidete nyie ndio kitovu cha maendeleo katika ofisi za Serikali. Jibu: Ofisi ya Rais, Utumishi - Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa inatambua kuwa utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za taifa ni jambo linalohitaji michango ya wadau mbalimbali katika utekelezaji wake. Michango hiyo hutegemewa sana na Idara ili kuleta mabadiliko chanya katika fani hiyo. Hivyo, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ipo tayari wakati wote kushirikiana na wadau mbalimbali ili kupata michango yao ambayo ni muhimu katika kuboresha utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka. Baadhi ya maeneo ambayo Idara imeshashirikiana na wadau ni pamoja na kuanzishwa kwa kada ya Watunza Kumbukumbu, kuanzishwa kwa mafunzo ya Cheti na Diploma katika chuo cha Utumishi wa Umma, maandalizi ya miongozo na taratibu mbalimbali za utunzaji kumbukumbu na nyaraka kama vile Sheria na Kanuni za utunzaji kumbukumbu na nyaraka. Baada ya kuanzisha Kada ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka za Taifa, na kuanzishwa kwa mafunzo ya cheti na Diploma katika Chuo cha Utumishi wa Umma, Idara imekuwa ikihamasisha wakuu wa ofisi za Umma na watendaji wengine ili waweze kutambua umuhimu wa fani ya utunzaji wa kumbukumbu , hivyo kuweza kuipa thamani inayostahili. Hivi sasa suala la utunzaji wa kumbukumbu linazungumzwa katika ngazi mbalimbali za utendaji. Aidha watunza kumbukumbu na nyaraka hupelekwa mafunzo ya Cheti, Diploma pamoja na semina za utunzaji kumbukumbu. Pia watumishi hao hupandishwa vyeo baada ya kupata sifa zinazotakiwa. Swali/Maoni Tungependa kila mwisho wa mhula wa mafunzo (semester) wanafunzi tupelekwe National Archive kwa Mafunzo zaidi na tujue jinsi ya kutunza kumbukumbu katika Nyaraka za Taifa. Jibu: Ofisi ya Rais, Utumishi - Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa inawakaribisha wakati wowote wanafunzi wanaohitaji kujifunza zaidi kuhusu namna bora ya kuhifadhi Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Jambo la msingi linalotakiwa kufanyika ni kutoa taarifa mapema ili maandalizi yaweze kufanyika. Aidha baadhi ya Taasisi za elimu huomba na kuleta wanafunzi kwa ajili ya mafunzo hayo. S.L.P 76161 Simu. 0784856244 Swali/ maoni: Kwa kuwa kuna habari nyingi zimeingizwa kwenye mtandao kwa hali hiyo mishahara/matokeo ya mitihani vyote hivyo tunavipata kwenye mtandao, sasa tunaomba kuwa habari zinazohusu watu wenye ulemavu wa aina zote ziwekwe kwenye mtandao ili jamii iweze kuwaelewa jamii ya watu wenye ulemavu kupitia mitandao hiyo. Ofisi ya Rais - Utumishi kupitia Kitengo cha Anuai za Jamii inachukua hatua mbalimbali kushughulikia watu wenye ulemavu ambao ni watumishi wa umma. Hatua hizi ni pamoja na kuandaa Mwongozo kuboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wenye ulemavu katika utumishi wa umma. Jibu: Taarifa mbalimbali zinazohusu watumishi, wakiwemo watumishi wa umma wenye ulemavu zimewekwa katika tovuti ya Ofisi ya Rais-Utumishi. Taarifa hizo ni pamoja Mwongozo wa Huduma kwa Watumishi wa Umma wenye ulemavu, Watumishi waliopatiwa ufadhili wa Shahada ya pili kwa mwaka 2008-2009 wakiwemo watumishi wenye ulemavu, tangazo kuhusu ufadhili wa Shahada ya pili kwa watumishi wanawake na watumishi wenye ulemavu na taarifa ya utekelezaji wa Mwongozo kuhusu huduma wanazotoa waajiri katika sehemu za kazi kwa watumishi wenye ulemavu. Ofisi ya Rais-Utumishi itaendelea kutoa taarifa mbalimbali kupitia tovuti, maonesho ya Saba Saba, maonesho ya Nane Nane, vipindi vya Radio na Luninga, pamoja na magazeti ili taarifa ziweze kuyafikia makundi yenye ulemavu. Simu: 0784505727/ 0715 505727 Swali/Maoni: kuna matumizi mabaya ya madaraka katika taasisi za Afya na Polisi. Jibu: Ofisi ya Rais-Utumishi imeanzisha mfumo wa malalamiko katika taasisi za umma kwa lengo la kuboresha huduma. Hivyo wananchi wanashauriwa kutumia mfumo wa malalamiko kuwasilisha kero/malalamiko yao. Mfumo huu tayari unatekelezwa Wizara ya Afya, Wizara ya Mambo ya Ndani, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Ofisi ya Rais-Utumishi, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Manispaa ya Ilala na Hospitali ya Amana. Mpango uliopo ni kwa mfumo huu kuwepo katika taasisi zote za umma. Hata hivyo, pale ambapo hakuna mfumo, kero zinaweza kuwasilishwa kwa Mkuu wa taasisi husika kwa kutumia barua, barua pepe, nukushi au kupitia vyombo vya habari na tovuti ya wananchi yenye anuani; www.wananchi.go.tz Simu: 0717583435 Swali/ maoni: Maadili kwa watumishi wa umma bado hayaridhishi japo kanuni za maadili kwa watumishi wa umma, (watumishi wanavujisha siri za Serikali, mavazi yasiyo rasmi, upendeleo kwenye kutoa huduma). Tuna shauri ofisi za maadili zifunguliwe katika ngazi ya Wilaya na Mkoa Jibu: kwa mujibu wa sheria namba 8, ya utumishi wa umma ya mwaka 2002, kifungu cha 35 sehemu ya 2 (a) waajiri wamepewa mamlaka ya kushughulikia masuala yote ya maadili na nidhamu kwa watumishi. Hivyo jukumu la kusimamia maadili kwa watumishi wa umma linapaswa kushughulikiwa na kila mwajiri. Hivyo endapo kuna masuala ya ukiukwaji wa maadili kwa watumishi waajiri katika ngazi ya wilaya wanapaswa kushughulikia. S.L.P 169, Songea. Swali/ maoni: Wananchi mikoani hawajui ni vipi watatoa malalamiko yao pindi kunapopatikana matatizo. Jibu: Ofisi ya Rais-Utumishi imeanzisha mfumo wa kushughulikia malalamiko ambao tayari unafanya kazi katika taasisi saba za umma. Mpango wa utekelezaji uliopo kwa sasa ni kueneza mfumo huu katika taasisi zote za umma. Hata hivyo, pale ambapo hakuna mfumo, kero zinaweza kuwasilishwa kwa Mkuu wa taasisi husika kwa kutumia barua, barua pepe, nukushi au kupitia vyombo vya habari na tovuti ya wananchi yenye anuani; www.wananchi.go.tz Swali/ Maoni: Kwanza kabisa napenda kushukuru kwa Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Umma. Napendekeza Mtumishi yeyote anapomaliza makato yake kama vile NSSF kwenda masharti ya kudumu anaposubiri mpaka kustaafu pesa haiwezi kumsaidia/ kusomesha au kujikimu (thamani inakuwa imesisha). Simu No. 0756625737 Jibu: Nia ya Serikali kuanzisha Mifuko ya Mafao ya Pensheni na Hifadhi za Jamii ni kuwawezesha watumishi wake, waweze kupata mafao mazuri yatakayowawezesha kumudu maisha yao kwa urahisi pindi wanapostaafu au kukoma utumishi wao. Kwa mujibu wa Sheria ya NSSF Cap. 50 R.E. 2002 Sehemu ya 5 inayohusu Mafao ya Watumishi wanaochangia NSSF, na kwa mujibu wa Vifungu 21, 22, 23, vya Sheria hiyo ili mtumishi aweze kulipwa mafao lazima awe ametimiza miaka 55 au 60. Hivyo basi kwa kuzingatia sheria hiyo Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii unao utaratibu wa kuhifadhi mafao ya watumishi wanaobadilisha masharti ya kazi kutoka “Operational Service” kwenda “Permanent and Pensionable” mpaka hapo mtumishi atakapofikisha umri wa kustaafu. Aidha, mafao hayo hulipwa pamoja na “bonus” ili kuepuka ‘devaluation’ ya fedha zilizoifadhiwa kwa muda mrefu. |