|
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma Mhe. Hawa A. Ghasia (MB) amesema Serikali imeanzisha matumizi ya Mikataba ya Huduma kwa Mteja na Upimaji wa wazi wa utendaji kazi (OPRAS) ili kujenga misingi thabiti ya kutoa huduma kwa wananchi na kuondoa ubabaishaji. soma zaidi ...
Waziri Ghasia alisema hayo wakati wa ufunguzi wa semina shirikishi kuhusu mabadiliko katika utumishi wa umma iliyoshirikisha watendaji na wadau muhimu wanaowahudumia wananchi, mkoani Iringa na Singida. Mhe. Ghasia alisema kuwa mifumo hiyo imewekwa na serikali ili kuwapima watumishi wake kwa malengo wanayojiwekea kwa mwaka na viongozi wao ili kila mtumishi ajue anakwenda ofisini kufanya nini. Waziri Ghasia alisema ili kufanikiwa kwa mikataba ya Huduma kwa Mteja, wananchi wanatakiwa wawe na uelewa wa hali ya juu wa mikataba yenyewe, kuelewa huduma zinazotolewa na taasisi husika, namna ya kuzipata huduma hizo, wajibu wao katika kuzipata huduma hizo na namna ya kulalamika pale ambapo hawapatiwi huduma hizo. Hata hivyo, Mhe. Ghasia aliainisha kuwa mambo hayo muhimu bado hayajaeleweka hivyo kuna kila sababu ya serikali kuchukua hatua za dhati za kuwajengea wananchi pamoja na watumishi wa umma uelewa. Pamoja na hayo, alifafanua kuwa waajiri wanatakiwa kutoa msisitizo wa matumizi ya mfumo wa upimaji utendaji kazi kwa uwazi kwa watumishi wa umma ili waweze kutekeleza yale yaliyoahidiwa katika mikataba ya huduma kwa mteja kwa haraka na ufanisi zaidi. Pia, watumishi wa umma wanatakiwa wafundishwe namna ya kujaza fomu za kuwapima utendaji kazi na kufahamu malengo ya kazi wanayotakiwa kuyatekeleza. Waziri Ghasia alikumbusha dhana ya kuwa na maisha bora kwa kila Mtanzania ambayo imo ndani ya ilani ya Chama Cha mapinduzi (CCM), na mbayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete amekuwa akiisisitiza tangu aingie madarakani ili iweze kufikiwa ni vyema kila mtumishi wa umma kuwajibika. Alisema Watumishi wa umma wanatakiwa kufuata maadili ya utumishi wa umma kwa kuacha uongo, utoro kazini, wizi, kupokea rushwa, kutoa huduma kwa upendeleo na mengineyo ambayo ni ukiukwaji wa maadili. Mhe. Ghasia alisisitiza waajiri wasisite kuwachukulia hatua za kinidhamu watumishi wa umma wasiokuwa na maadili, pia aliwaagiza watendaji wakuu wote wa ofisi za Serikali kuangalia vizuri ajira za watumishi wao iwapo kuna watumishi wasiokuwa na sifa. Semina hiyo, pamoja na wengine, ilihudhuriwa na viongozi wa ngazi mbalimbali wa mikoa, viongozi wa vyama vya siasa, viongozi wa Dini, na watendaji wa mashirika yasiyo ya kiserikali. Semina shirikishi kuhusu mabadiliko katika utumishi wa umma zimeshafanyika katika wilaya zote za mikoa ya Manyara, Kigoma, Rukwa, Ruvuma, Mtwara, Lindi na Pwani. |