|
Makamu wa Rais, Dk. Ali Mohamed Shein amesema utoaji wa huduma za umma katika Bara la Afrika utaweza kuimarika ikiwa Serikali zitashirikiana na wahusika mbalimbali ambao ni pamoja na Serikali za Mitaa, asasi zisizo za kiserikali, mashirika ya kidini na sekta binafsi. Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika katika viwanja vya Mnazi mmoja jijini Dar es salaam. Tafadhali soma hotuba kamili, inaendelea...
HOTUBA YA MHESHIMIWA DK. ALI MOHAMED SHEIN, MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA KWENYE KILELE CHA SHEREHE ZA SIKU YA UTUMISHI WA UMMA YA BARA LA AFRIKA TAREHE 19 JUNI 2009 VIWANJA VYA MNAZI MMOJA, DAR ES SALAAM Mheshimiwa Dalmas O. Anyango, Mwenyekiti wa Mkutano wa Sita wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma Barani Afrika; Mheshimiwa Kajura Henry Muganwa, Naibu wa Waziri Mkuu na Waziri wa Utumishi wa Umma, Jamhuri ya Uganda; Mheshimiwa Hawa A. Ghasia, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma; Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri; Mheshimiwa William Lukuvi;Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mheshimiwa Julia Doly Joiner, Kamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika; Waheshimiwa Wabunge; Makatibu Wakuu; Wawakilishi wa Nchi na Mashirika ya Kimataifa, Watendaji wa Serikali, Washiriki wa Maonyesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Wageni waalikwa, Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana. Napenda kuanza kwa kuelezea furaha yangu ya kualikwa hapa ili nijumuike nanyi, Ndugu Wananchi, katika maadhimisho haya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika, ambayo yamefikia kilele chake leo.Nachukua fursa hii kukushukuru wewe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Mh. Hawa A. Ghasia, kwa kunipa heshima ya kuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya Siku hii muhimu katika medani ya utumishi wa umma katika Bara letu. Nakupongeza kwa uongozi mzuri ulioiwezesha Tanzania, ikiwa mwenyeji, kuzifanikisha sherehe za maadhimisho haya ya mwaka huu ya Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika. Nafahamu kuwa kupanga, kuandaa na kusimamia shughuli zinazohusiana na maadhimisho kama haya sio kazi ndogo.Natoa hongera zangu nyingi kwani, tunapofikia kilele chake hivi leo, kwa hakika maadhimisho haya yamefana sana pamoja na kauli yake mbiu yake inayotuhimiza “Kuimarisha Ushirikiano Thabiti Baina ya Serikali na Wadau katika Utoaji Huduma na Kuleta Maendeleo Endelevu Barani Afrika’’. Lakini nachukua fursa hii pia kuwashukuru wale wote ambao, kwa namna moja au nyingine, wamesaidia katika kufanikisha maadhimisho haya, pamoja na sherehe zilizoambatana nayo. Naushukuru Umoja wa Afrika kwani ndio uliobeba jukumu la kuhakikisha kuwa maadhimisho haya ya Siku ya Utumishi wa Umma katika Bara letu yanafanyika. Vile vile napenda kuushukuru Mkutano wa Mawaziri wa Utumishi wa Umma uliofanyika Windhoek nchini Namibia, mwaka 2007, kwa kuichagua nchi yetu kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Utumishi wa Umma ya Bara la Afrika, mwaka huu. Kwa hakika, hii ni heshima kubwa, na Tanzania imefarijika kuwa mwenyeji wa maadhimisho haya yaliyohudhuriwa na Waheshimiwa Mawaziri wenye dhamana kubwa ya utumishi wa umma katika Bara letu. Shukrani zangu nyingine ziende kwa wizara, idara na mashirika ya humu nchini na nje ya nchi kwa kuweza kushiriki kikamilifu katika shughuli zilizofanyika wakati wa Wiki ya Utumishi wa Umma mwaka huu 2009. Nina furaha kukufahamisheni Ndugu Wananchi kuwa sherehe hizi, hapa leo, zimehudhuriwa pia na Waheshimiwa Mawaziri na Manaibu Mawaziri watano wenye dhamana hio ya Utumishi wa Umma kutoka nchi nyingine za Afrika. Naomba niwataje nikianza na: 1. Mheshimiwa Kajura Henry Muganwa kutoka Uganda, 2. Mheshimiwa Dalmas Otieno Anyango kutoka Kenya, 3. Mheshimiwa Richard Baloyi kutoka Afrika ya Kusini, 4. Mheshimiwa Profesa E. G. Mukonoweshuru kutoka Zimbabwe, 5. Mheshimiwa Amany Essawi kutoka Misri. Lakini napenda nimtaje pia Mheshimiwa Julia Joiner, Kamishna wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoka Addis Ababa Ethiopia. Kwa niaba ya wananchi na kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kukuhakikishieni kuwa sisi katika nchi hii tumefurahi kuwa mmeweza kuungana nasi kusheherekea Siku hii ya Utumishi wa Umma ya Afrika hapa Dar es Salaam. Pamoja na kukukaribisheni, nina hakika kuwa mmepokewa kwa ukarimu unaostahiili na mwenyeji wenu, Waziri wa Nchi wa Utumishi wa Umma, Mheshimiwa Hawa A. Ghasia, na kuhakikisha kwamba mnapata huduma zote muhimu za kuwawezesha kufurahia uwepo wenu hapa nchini petu. Kwa mara nyingine nasema “karibuni sana Tanzania”. Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Tunaposherehekea Siku hii muhimu, naamini tunaukumbuka pia usemi wa busara wa profesa mmoja wa Uingereza, kwamba, nanukuu: ‘’Utawala ni zaidi ya Serikali na watumishi wake. Ni kuhusu utoaji wa huduma kwa walio maskini sana. Aidha utawala ni kuwapa wananchi uwezo wa kuchangia katika mambo yanayowahusu.’’ Kwa maana hio, tunaposema kwamba leo ni Siku ya Utumishi wa Umma tunamaanisha kwamba hii ni siku ya ninyi, Ndugu Wananchi, zaidi kuliko wale walio katika utumishi wa umma. Hii siku inatupa sote nafasi adhimu ya kutathmini fursa na changamoto ambazo watumishi wa umma wanakumbana nazo katika harakati za kuimarisha maisha ya wananchi tunaowatumikia. Kwa sababu hio, ni muhimu tukakumbuka kwamba utumishi wa umma duniani kote ni kazi ya wito inayohitaji ustahimilivu na kutambua pia umuhimu wa utoaji kwa wananchi. Ingawa neno ‘’mtumishi’’ halitumiki tena katika viwanda na makampuni ya sekta binafsi katika Utumishi wa Umma hili ni neno lenye kubeba maana yake halisi, kwani linaelezea kazi tunazozifanya katika utumishi huo. Kwa hakika, sisi katika utumishi wa umma tupo kwa ajili ya kuwatumikia Wananchi. Kwa hivyo, siku ya leo ni fursa tunayopaswa kuitumia vyema katika kutafakari kuhusu utumishi wetu ili tufahamu kama tunatosheleza matakwa na shida za wateja wetu ambao ni wananchi. Vile vile hii ni nafasi ya kuangalia kuwafikia na kuwashirikisha Wananchi katika mambo yote tunayoyafanya, na mipango yetu ya baadaye tunayoiweka ya kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Ni lazima kila tunaposherekea Siku hii ya Utumishi wa Umma tuitambue nafasi pekee ya Utumishi wa Umma, yenye ufanisi na tija, katika kulikomboa Bara letu kutokana na lindi la umasikini katika karne hii ambayo inaelezwa kuwa ya Bara la Afrika. Hakuna muda mwengine isipokuwa katika siku hii ndio wakati unaotubidi tutambue kuwa maendeleo ya Bara letu hayataweza kupatikana kwa njia nyengine bila ya kuwa na watumishi wa umma ambao ni wachapa kazi, wenye kujituma wenye ari ya kujitolea. Ni kwa sababu hio, malengo makuu ya uimarishaji wa utumishi wa umma ni pamoja na kuwa na watumishi wa kutosha, watumishi wenye maadili mema, na watumishi wanaowajibika vilivyo katika kutoa huduma bora pamoja na kufanya kazi nyengine za umma. Watumishi wa umma wanaotambua wajibu wao ni lazima watakuwa ni watu wanaoichukia na kuikemea tabia mbaya ya baadhi ya watumishi wenzao wenye mwenendo unaokuwa ni kinyume na utumishi bora. Tabia zinazoleta aibu na fedheha zinachafua sifa ya utumishi wa umma wote mbele ya wananchi. Ni lazima watumishi bora wawachukie na wawakatae watumishi wote wa umma ambao hawana maadili mema, na wasiowajibika ipasavyo. Kwa hakika masuala mengi ya ukiukaji wa maadili yanatokana na uwajibikaji mdogo wa watumishi, usimamizi mbaya na mifumo dhaifu ya utawala. Fursa nzuri kwetu ya kusahihisha mambo yote yanayojitokeza, na kuonekana yana upungufu huo, ni wakati huu tunaposheherekea Siku hii ya Utumishi wa Umma Barani Afrika. Lakini ninaamini pia kuwa Siku hii ya Utumishi wa Umma inatupa fursa vile vile ya kutambua umuhimu wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma. Kwa maana hio, hii ni siku ya kukumbushana kuwa rasilimali watu ni rasilimali yenye thamani kubwa katika Nchi yoyote ile. Hii inatokana na ukweli kwamba Rasilimali Watu yenye ubora, tija na ari ya kufanya kazi ni muhimu katika utawala, uzalishaji na usambazaji wa bidhaa na huduma kwa Wananchi. Rasilimali watu ni muhimu katika uandaaji na utekelezaji wa sera za uchumi, na katika usimamizi wa matumizi ya rasilimali nyingine za umma. Kwa hakika, bila ya kuwa na rasilimali watu iliyo makini, ni wazi kuwa demokrasia na maeneleo ya nchi hayatapatikana. Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana, Hakuna mjadala kuhusu ubora wa rasilimali watu kuwa ni nyenzo ya msingi katika maendeleo ya nchi yoyote duniani. Kwa maana hio, napenda kuwanasihi viongozi wa mpango wa uimarishaji wa utumishi wa umma wahakikishe kwamba watumishi wa umma wanapata mafunzo yatakayokidhi mabadiliko ya kiuchumi na kijamii yanayotokea katika nchi yetu. Wizara, idara na vyombo vingine vya umma havina budi kuandaa na kutekeleza mipango ya mafunzo na maendeleo ya rasilimali watu, kwa lengo la kujenga uwezo wa watumishi wa kada mbali mbali. Lakini muhimu pia ni kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanathaminiwa, wanatambuliwa, wanasaidiwa na wanaelimishwa kutokana na michango wanayoitoa katika kujenga utumishi wa umma uliotukuka. Ni lazima tutambue kwamba bila ya kuwa na watumishi wa umma wenye uwezo, ari, sifa, na wenye kufurahia wajibu wao wa kuwatumikia wananchi itakuwa vigumu kwa nchi zetu za Afrika kuyafikia malengo ya maendeleo ya milenia. Napenda niseme kwamba Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika ni wakati mzuri wa kuzitambua, na kuziheshimu kazi za ubunifu katika sekta ya Utumishi wa Umma. Ninaamini kuwa nyote mnafahamu kuwa Umoja wa Mataifa uliamua kusherekea tarehe 23 Juni ya kila mwaka, kuwa ni siku maalum ya kuzitambua, na kuziheshimu faida za utendaji kazi wa pamoja, ubunifu na usikivu wa sekta ya utumishi wa umma. Kwa hivyo, leo nasi katika Bara la Afrika, ni siku ambayo watumishi, na vyombo vya umma, vinatukuzwa kutokana na kazi zake nzuri za kupigiwa mfano kwa sababu ni kazi zinazoimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi. Kwa hakika, watumishi wa umma wa namna hio ndio kielelezo kikubwa cha uimara na ubora wa sekta ya Utumishi wa Umma. Bila shaka yoyote wananchi wanaopata huduma nzuri wanazifurahia, lakini vile vile wanajivunia kuwa na Watumishi wa umma wanaowajibika wa namna hio. Kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri Muungano wa Tanzania, kwa niaba yangu mwenyewe, napenda kutoa shukrani zangu za dhati kwa watumishi wa umma, kote Barani Afrika, kwa kazi nzuri ya kuwahudumia Wananchi ipasavyo. Lakini ninawapongeza watumishi walio bora, ninawatarajia kuendeleza ari hio ili kazi zao zizidi kuwa bora na mfano wa kuigwa na watumishi wengine waweze na wao kuuenzi utumishi bora wa umma. Kila mtumishi wa umma anapaswa kuendeleza uwajibikaji wake, maadili mema, usikivu, weledi, na utendaji mzuri wa kazi ili utumishi wa umma ujali zaidi matokeo ya kazi za umma badala yale wenye ubinafsi. Aidha juhudi na mifano hiyo ya utumishi bora pia itaweza kuwachochea watumishi wengine ili na wao wawe wabunifu wakati wa kutekeleza sera na mikakati iliyowekwa na Serikali zetu. Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa, Mabibi na Mabwana, Napenda kuchukua nafasi hii nizungumze machache kuhusu Kauli Mbiu ya Siku ya Utumishi wa Umma ya Bara la Afrika ya mwaka huu. Kwa hakika ujumbe wa kauli mbiu hio una umuhimu wake katika hali halisi ya hivi sasa khususan unapotutaka : ‘’Kuimarisha ushirikiano thabiti baina ya serikali na wadau katika utoaji huduma na kuleta maendeleo endelevu Afrika’’ Ni ukweli usiopingika kwamba utoaji wa huduma za umma katika Bara la Afrika utaweza kuimaimarika ikiwa Serikali za nchi zetu zitashirikiana na wahusika mbali mbali ambao ni pamoja na serikali za Mitaa, Asasi zisizo za kiserikali, mashirika ya kidini na sekta binafsi. Umuhimu wa ushirikiano huu unatokana na sababu zifuatazo: (i) Mabadiliko katika tabia za Wananchi ambao matarajio yao kutoka kwa utumishi wa umma yanazidi kuongezeka; (ii) Wananchi na watumiaji wa huduma za umma wanazijua haki zao na wanadai uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma. Hali hii inatokana na kukua kwa mwamko kufuatia msukumo wa kijamii na vyombo vya habari; (iii) Pamoja na kutakiwa kuongeza ubora wa huduma, sekta ya utumishi wa umma inakabiliwa na changamoto za upungufu wa bajeti ambao hauwezi kuendelea kuzibwa kwa vyanzo vya kodi; (iv) Kuna ushindani mkubwa baina ya Nchi mbali mbali zinazoendelea na zilizoendelea katika kuvutia vitegauchumi na wawekezaji. Kutokana na sababu hizo na uwazi kwamba utoaji wa huduma utaweza kuimarika ikiwa utawashirikisha watoaji huduma wengine. Nchi za Afrika hazina budi sasa kujihusisha zaidi na shughuli muhimu ambazo ni majukumu ya dola zikiwemo ulinzi, usalama na miundombinu. Katika masuala mengine, nchi zetu zishirikiane na wahusika wengine katika kutoa huduma hizo. Ninafurahi kukufahamisheni kuwa Tanzania imekuwa ikitekeleza kauli mbiu ya ’Kuimarisha ushirikiano thabiti baina ya serikali na wadau katika utoaji huduma na kuleta maendeleo endelevu Afrika’’. Kupitia Programu ya Mabadiliko katika Utumishi wa Umma, Serikali ya Tanzania imepanua wigo wa kutoa huduma kwa Wananchi kwa kuwatumia wahusika mbali mbali ikiwemo Serikali Kuu, Serikali za Mitaa, Wakala za Serikali, Asasi zisizo za kiserikali na Sekta binafsi. Hivi sasa, uwezekano wa kupanua ushirikano kati yake na sekta binafsi katika utoaji wa huduma kubwa zikiwa ni pamoja na uimarishaji wa miundombinu, ukiowemo ujenzi, na ukarabati wa barabara, bandari, na utoaji wa huduma muhimu za maji na umeme. Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Mabibi na Mabwana, Kabla ya kuhitimisha hotuba yangu, napenda sote tuchukue fursa ya maadhimisho ya Siku hii kutafakari juuya aina ya Utumishi wa Umma ambao Bara letu la Afrika litapendelea kuuona ukijijenga na kujiimarisha katika nchi zetu kadri siku zinavyoenda. Lakini ninaamini Mkataba wa Utumishi wa Umma Barani Afrika uliopitishwa na Mkutano wa Mawaziri wa Afrika wa Utumishi uliofanyika Windhoek nchini Namibia mwaka 2001 utaweza kutusaidia na kutuongoza katika kuupata utumishi wa umma tunaoutaka. Mkataba huu unatilia kazi muhimu za utumishi wa umma katika kuleta maendeleo na demokrasia na unautaja utumishi wa umma kuwa ni injini ya kuleta maendelea ya kiuchumi, khususan kwa kutumia teknolojia mpya na ya kisasa. Hakuna ubishi kwamba sote tunapenda kuona kuwa tunakuwa na utumishi wa umma ulio imara, wenye ufanisi wa hali ya juu, unaokubalika, na unaoendeshwa kisheria. Tunapenda tuwe na utumishi wa umma unaotoa huduma kwa kasi, na kwa usikivu wa hali ya juu. Tunapenda kuuona utumishi wa umma huo unajali viwango, na muda wa utoaji wa huduma. Aidha, utumishi wa umma ulio bora ni ule ambao misingi yake ni weledi na maadili mema. Viwango vya maadili hayo ni pamoja na tabia nzuri na utoaji wa huduma bila kujali tofauti za itikadi. Hatuna budi, hata hivyo, tukubali kuwa utumishi wa umma katika Bara letu la Afrika una changamoto kubwa, hasa zinazotokana na muingiliano wa utandawazi. Hali hio inaleta viwango na mambo mengi mapya yanayogusa utumishi wa umma ambayo inabidi yafanyiwe kazi ili yaendane na mazingira yetu. Waheshimiwa Mawaziri, Wageni Waalikwa, Ndugu Wananchi, Nimalizie kwa kutoa shukrani zangu za dhati, kwa mara nyengine, kwa kupewa heshima kubwa kuzungumza nanyi, ndugu wananchi, wakati huu tunapohitimisha maadhimisho haya muhimu. Lakini napenda kuchukua tena nafasi hii kusisitiza juu ya msemo wa taasisi ya AAPAM, unaozungumzia kwamba tukiwa watumishi wa umma: ‘’Hatutamnyima mtu yeyote huduma’’; ‘’Hatutakawiza huduma kwa mtu yeyote’’; ‘’Hatutaharibu huduma kwa mtu yeyote’’ Ni maneno muhimu ya kukumbushana katika sherehe hizi za Siku ya Utumishi wa Umma. Baada ya kuyaeleza hayo, naitakia kheri Siku ya Utumishi wa Umma Barani Afrika, na mafanikio endelevu katika siku zijazo.Ndugu wananchi, nakushukuruni sana kwa kunisikiliza kwa makini. Akhsanteni “Afrika” |